Waziri wa Afya wa Brazil Nelson Teich amejiuzulu wadhfa wake, ikiwa si zaidi ya mwezi mmoja tangu akalie kiti hicho, kutokana na kile kilichoelezwa utata uliomo ndani ya serikali ya taifa hilo katika namna ya kulishughulikia janga la virusi vya corona.

Akizungumza mjini Brasilia, pasipo kueleza sababu za uamuzi wake huo, Teich alisema maisha yanajumuisha uamuzi na sasa ameamua kuondoka.

Lakini kwa mujibu wa chombo kimoja cha habari nchini humo ni kwamba awali alikutana na Rais wa Brazil Jair Bolsonaro.

Waziri huyo anatajwa kuupinga mpango wa Bolsonaro wa kurefusha matumizi ya dawa ya malaria ya hydroxychloroquine kama tiba ya COVID-19, akionya itaweza kusababisha madhara zaidi.

Vilevile alikuwa akiupinga msukumo wa rais huyo, wa kufungua zaidi vyanzo vya uchumi, ukiwemo uamuzi wa kufungua saluni za urembo, kunyoa nywele pamoja na vituo vya michezo.

Mtangulizi wa Teich, Luiz Henrique Mandeta alijiuzulu kutokana na sababu kama hizo aliposhindwa kukubaliana na Rais Bolsonaro.

Brazil yenye jumla ya watu milioni 200, ina maambukizi 206,000 na vifo 14,000 na kuifanya kuwa taifa la sita lenye vifo na maambukizi mengi duniani.

The post Waziri wa Afya, Brazil ajiuzulu baada ya mwezi mmoja kazini  appeared first on Bongo5.com.