SALVATORY NTANDU
Imebainishwa kuwa Mikopo yenye riba ya juu na isiyokuwa na mikataba inayotozwa na Taasisi za Kifedha mkoani Shinyanga inachangia kukwamisha utendaji kazi wa Walimu katika Vituo vyao vya kazi kutokana na baadhia yao kudaiwa na taasisi hizo.
Hayo yamebainishwa Mei 14 mwaka huu na katibu wa Chama cha Walimu Manispaa ya Shinyanga, James Peter katika Mkutano (CWT) uliofanyiaka Mjini humo na kufafanua kuwa ofisi yake inamashauri mengi yenye malalamiko ya walimu kudaiwa fedha na Vikundi vya ukopeshaji fedha (SACCOS) pamoja na baadhi ya Mabenki .
Alisema kuwa wengi wao wanatozwa riba za juu ambazo zinasababisha washindwe kufundisha kwa ufanisi katika vituo vyao vya kazi hali ambayo imekuwa ikisababisha migogoro isiyokuwa na tija na waajiri wao pindi wanapofanyiwa ukaguzi.
“Tumebaini Kuna walimu wamekopeshwa fedha na Taasisi hizi bila ya kuwa na mikataba ya ukopeshaji hali ambayo inasababisha waendelee kukatwa fedha kwa muda mrefu hata kama wamemaliza kulipa madeni yao,huku wengine wakidiriki kushikilia kadi zao za benki,”alisema James
James alifafanua kuwa ni wakati sasa wa Walimu mkoani humo kuitumia benki ya walimu ili kujipatia mikopo kwa riba nafuu ambayo itawasaidia kujikwamua kimaisha hususani katika kipindi hiki cha uwepo wa janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.
Awali akifungua mkutano huo, Katibu wa Cwt Mkoa wa Shinyanga,Mwalimu Lazaro Tuliasaulo aliwataka walimu kuachana na mikopo isiyokuwa na tija sambamba na kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi ya maendeleo ambayo inaweza kuwapatia fedha za kujikimu.
“Tumieni kipindi hiki ambacho shule zimefungwa kutokana na COVID 19 kuaibua miradi ya ujasiriamali itakayowawezesha kupata fedha achaneni na mikopo ambayo inasababisha mfukuzwe kazi na waajiri wenu tumieni maarifa mliyonayo katika vituo vyenu vya kazi kujipatia fedha kwa njia zilizo halali,”alisema Tuliasaulo.
Nae Raymond Shimiyu Mwalimu kutoka shule ya sekondari Mwisela amewaomba walimu kutumia asilimia 15 ya fedha zinazotolewewa na CWT kwa matawi katika vituo vyao vya kazi kwa kuanzisha miradi ya maendeleo na kuachana na tabia ya kuzigawana fedha hizo ambazo zinaweza kuwasaidia.
“Fedha hizi zinatosha kuanzisha miradi ya ufugaji,kilimo na viwanda vidogo naomba CWT itoe mwongozo ili zitumike kama ilivyokusudiwa maana kwa sasa huwa tunazigawana katika shule zetu pindi zinapotolewa,”alisema Shimiyu.
Zaidi ya walimu 50 wanadaiwa fedha mbalimbali na taasisi hizo ambapo wanasheria wa CWT wanaendelea kuyahakiki madeni hayo ili kujiridhisha na uhalali wake kutokana na baadhi yao kubainika kuendelea kukatwa fedha licha ya kumaliza madeni yao.
mwisho