KUJIPATIA FEDHA KWA NJIA YA UDANGANYIFU [MTANDAO WA KIJAMII].

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili 1. SOPHIA ELIA MWALUANDA [22] Mfanyabiashara na Mkazi wa Sistila Jijini Mbeya na 2. MPAJI SELEMAN MWINYIMVUA [38] Mkazi wa Manzese Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kutumia akaunti feki ya “facebook” yenye jina la Mheshimiwa Mama Janeth Magufuli Mke wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli.

Watuhumiwa wamekamatwa mnamo tarehe 28.04.2020 majira ya saa 15:00 Alasiri katika operesheni na msako uliofanywa huko eneo la Ikuti Sokoni, Kata ya Ikuti, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya.

Mbinu wanayoitumia watuhumiwa ni kufungua akaunti “facebook” yenye jina la JANETH MAGUFULI SACCOS na kuuaminisha umma kwa kuweka picha ya mama Janeth Magufuli na kisha kutangaza kutoa mikopo nafuu kwa sharti la muombaji kutuma kwanza fedha kiasi cha Shilingi 76,500/= kwenye namba ya simu waliyoiweka kama ada ya mkopo ili aweze kupata mkopo wa Shilingi Milioni 3,000,000/=.

Watuhumiwa wamekutwa na simu mbili aina ya Infinix Smartphone ambayo imetumika kufungulia akaunti hiyo ya “facebook” na simu aina ya Siccoo Mobile [Analogue] inayotumika kupokea fedha zinazotumwa na watu mbalimbali. Aidha watuhumiwa wamekutwa na fedha taslimu shilingi 470,000/= ambazo wamekiri kuzipata kwa njia ya udanganyifu kupitia akaunti hiyo feki.

Mtakumbuka Februari 21, 2020 huko katika Mji Mdogo wa Mbalizi Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya liliwakamata vijana kumi na moja [11] kwa tuhuma za kujihusisha na wizi kwa njia ya mtandao kwa kutumia akaunti feki za mitandao ya kijamii ikiwemo “facebook” wenye majina ya viongozi wa Serikali na Wasanii maarufu wa hapa nchini. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

WITO WA KAMANDA.

Natoa rai kwa watanzania kuheshimu ikulu kwani ni mahali patakatifu na hapachezewi kabisa, Chombo cha dola hakitavumilia kuona mtu wa aina yeyote kwa vyovyote vile akitumia jina la ikulu kuibia au kutapeli watu wengine.

Ninatoa wito kwa wananchi kuwa makini na taarifa mbalimbali zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinaelekezea fursa mbalimbali kama vile ya mikopo, masomo na biashara ambazo zinawataka kutuma kiasi kadhaa cha fedha ikiwa ni moja ya masharti ya kupata fursa hiyo, ni vyema kujiridhisha kwenda mamlaka za serikali zilizo karibu kwa ajili ya kupata uhakika kabla ya kufikia uamuzi wa kutuma fedha.

Aidha ninawataka vijana kujenga utamaduni wa kufanya kazi ili kujipatia kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu ambavyo vitawasababisha kupata adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

Mwisho, ninatoa rai kwa mtu/watu waliotuma fedha kupitia namba ya watuhumiwa kwa lengo la kupata mkopo kufika kituo cha Polisi kilichopo jirani kwa ajili ya kutoa taarifa ili taratibu za kisheria zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa.

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA MAUAJI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wanne 1. RIZIKI ANTHONY MUHEMA [20] Mkazi wa Mtakuja Mbalizi, 2. REHEMA KASELA [36] Mama Mzazi wa marehemu na Mkazi wa Iwindi 3. ESTA MSONGOLE [52] Mganga wa Kienyeji na Mkazi wa Sumbawanga na 4. MTUMWA HAONGA [65] Mganga wa Kienyeji na Mkazi wa Mtakuja Mbalizi kwa tuhuma za mauaji ya mtoto TAMALI SIMON, miaka miwili na miezi mitatu.

Watuhumiwa walikamatwa katika operesheni maalum iliyofanywa na kikosi kazi cha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya tarehe 06.05.2020 majira ya saa 04:00 usiku huko Iwindi, Kata ya Utengule Usongwe katika Mji Mdogo wa Mbalizi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao ambao wamekiri kufanya tukio hilo kwa kushirikiana na mama mzazi wa marehemu.

Chanzo cha tukio ni tamaa ya kupata utajiri kwa njia za kishirikina baada ya mtuhumiwa ambaye ni mganga wa kienyeji kuwapa masharti yaliyopelekea kifo cha mtoto huyo.

Awali mnamo tarehe 04.05.2020 majira ya saa 20:00 usiku huko Kijiji na Kata ya Iwindi, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya, Mtoto TAMALI SIMON, miaka miwili na miezi mitatu, Mkazi wa Iwindi alikutwa ameuawa kwa kunyongwa shingo na mtu asiyejulikana na mwili wake kutelekezwa.

Kutokana na tukio hilo, Kikosi kazi cha Polisi Mkoa wa Mbeya kilifanya msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa katika maeneo tofauti na katika mahojiano watuhumiwa wamekiri kuhusika kwenye tukio hilo baada ya kupewa masharti na mganga wa kienyeji. Aidha upekuzi umefanyika nyumbani kwa Mganga wa kienyeji na kukamata vifaa mbalimbali vya uganga na dawa za kienyeji za aina mbalimbali. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA TUKIO LA MAUAJI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wanne 1. VIOLETH SIMELUTA [26] Mwalimu na Mkazi wa Isanga, 2. CHARLES SIMELUTA [39] Mkazi wa Isanga, 3. EMMANUEL KIWALE [30] Mkazi wa Mafiati na 4. SOPHIA SAMSON [42] Mkazi wa Airport ya Zamani kwa tuhuma za mauaji ya JUNIOR CHARLES MACHIBYA [30] Mkazi wa Airport ya Zamani.

Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 07.05.2020 baada ya kikosi kazi cha Polisi Mbeya kufanya msako na upelelezi wa kina na kubaini kuwa marehemu aliuawa kwa kupigwa vitu butu usoni na kunyeshwa sumu huku chanzo cha tukio hilo kikiwa ni ugomvi wa kifamilia.

Awali mnamo tarehe 30.04.2020 majira ya saa 20:00 usiku huko Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya JUNIOR CHARLES MACHIBYA [30] Mkazi wa Airport ya Zamani alifikishwa Hospitalini hapo na wasamalia wema wakidai kuwa amekutwa maeneo ya nyumbani kwake akiomba msaada na akilalamika maumivu makali ya tumbo akidai kuwa amenyweshwa sumu bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Tarehe 01.05.2020 majira ya saa 18:00 jioni alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu na ndipo upelelezi ulianza pamoja na msako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo. Upelelezi unaendelea.