Wanawake wa Mpwayungu, Mlowa barabarani na Mlowa Bwawani Wilaya ya Chamwino mkoani hapa wametaka elimu zaidi ili kuweza kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni, huku wakitaja tukio la mtoto wa kike kuozeshwa kwa mahari ya kiroba cha mkaa na nguruwe mmoja.

Pia wamewataka wazazi kuacha tamaa ya kuozesha watoto wao wakiwa na umri mdogo kwa lengo la kupata mali, hasa mifugo bila kujua wanaharibu maisha ya watoto hao.

Wakizungumza na HabariLEO hivi karibuni, walisema vitendo vingi vya kikatili ikiwemo kuwaoza watoto kwa tamaa ya kupata mali vimeshamiri na kufanya watoto kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu. Mkazi wa Mpwayungu, Magreth Ndosi alisema kuna watoto wa kike wamekuwa wakiozwa mara baada ya kumaliza elimu ya msingi.

Alisema katika tukio lililotokea hivi karibuni mzazi mmoja alimuoza binti yake kwa mahari ya kiroba cha mkaa na nguruwe mmoja.

Alisema baadhi ya wazazi wanaona mtoto akimaliza darasa la saba keshakuwa mkubwa, anastahili kuolewa bila kujali umri kwani anajua hawezi kushtakiwa.

Alisema wengi wanafahamu hawaruhusiwi kuoza watoto wanapokuwa shuleni lakini anapomaliza shule ya msingi akiwa na miaka hata wa miaka 15 anaona anastahili kumuozesha.

“Yaani mtu hafikirii maisha ya mtoto wake, wengi wanajali mifugo, anaona kiroba cha mkaa na nguruwe kina thamani ya maisha ya mtoto wake,” Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha watoto kulea watoto wenzao.

“Ukitembea huku vijijini utaona mtoto ana mtoto na limekuwa ni jambo la kawaida” alisema

Mkazi wa Mlowa barabarani, Damaris Mchile alisema tabia ya wazazi kutoona umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike inachangia watoto wa kike kukosa fursa ya kupata elimu au wale wanaopata elimu wakiishia darasa la saba inaonekana imetosha.

Baadhi ya wananchi wa maeneo hayo walipatiwa mafunzo ya kuwa waelimisha rika kwenye mradi uliotekelezwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Woman Wake Up (Wowap) ambalo hujishughulisha ushawishi na utetezi hasa wanawake na watoto.

Mratibu wa mradi huo, Nasra Suleiman alisema bado elimu inahitajika ili kuweza kubadili mitazamo na kuacha kuwaoza watoto wakiwa na umri mdogo. Alisema bado watoto wa kike wanachukuliwa kama kitega uchumi katika kujipatia mali bila kujali hatma ya watoto hao.

Source: Habari Leo

The post Wanawake walaani tukio la mtoto wa kike kuozeshwa kwa mahari ya kiroba cha mkaa na nguruwe mmoja appeared first on Bongo5.com.