Tangu alipoingia madarkani Donald Trump huko Marekani, rais huyo mwenye majigambo mengi amekuwa akifuata siasa maalumu dhidi ya China na kuishinikiza Beijing katika pande mbalimbali. 

Hivi sasa na baada ya kuenea sana maambukizi ya kirusi cha corona na serikali ya Trump kulaumiwa sana kwa kufanya uzembe, kushindwa kukabiliana na maambukizi hayo na kuzitia hatarini roho za mamia ya maelfu ya Wamarekani, muda wote Trump amekuwa akisaka kondoo wa kuwatoa muhanga ikiwemo China. Trump sasa hivi ametoa vitisho vikali vya kukata kikamilifu uhusiano wa nchi hiyo na Marekani. 

Katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya FOX Business na kurushwa hewani juzi Alkhamisi, Trump alitishia kukata kikamilifu uhusiano wa Marekani na China. Alidai kuwa kukata uhusiano huo kutaifanya Marekani ihifadhi akiba kubwa sana ya fedha. Katika sehemu moja ya mahojiano hayo, Trump alisema: "Kuna kazi nyingi za kufanya. Tunaweza kukata uhusiano wetu wote. Sasa kama tutafanya hivyo, nini kitatokea? Kama tutakata kikamilifu uhusiano, tutaweza kuhifadhi dola bilioni 500..." 

Kusema kweli vitisho hivyo vya Trump vinaulenga moja kwa moja uhusiano wa kiuchumi wa Marekani na China wenye thamani ya mamia kadhaa ya mabilioni ya dola. Inaonekana wazi kwamba vitisho hivyo vya Trump zaidi ni upayukaji na ni sehemu za kampeni zake za uchaguzi zilizoathiriwa vibaya na maafa ya ugonjwa wa COVID-19 huko Marekani. Ni jambo lililo wazi kwamba kama Marekani itavunja kikamilifu uhusiano wake na China, basi mashirika, viwanda pamoja na mamilioni ya Wamarekani watakuwa hatarini kutokana na kutegemea kwao bidhaa kutoka China. 

Kiujumla ni kwamba mivutano baina ya Marekani na China inahusu nyuga mbalimbali; za kisiasa, kibiashara, kiuchumi, kijeshi, kiusalama, kiistratijia n.k. Washington inaiona China kuwa ni mpinzani wake mkubwa na inasisitiza sana kupambana na kasi ya maendeleo ya Beijing. Kwa upande wake China na Russia ni wapinzani wakuu wa siasa za Donald Trump za kujikumbizia kila kitu upande wake katika masuala ya dunia kama ambavyo Beijing inamlaumu vikali pia Trump kwa siasa zake za kuziwekea vikwazo na ushuru mkubwa bidhaa za nchi nyinginezo. 

Alaakullihaal, kuzuka wimbi la maambukizi ya kirusi cha corona kumeshadidisha mzozo baina ya China na Marekani. Trump na baadhi ya viongozi wa serikali yake ambao wanalaumiwa vikali kwa kufanya uzembe na kushindwa kutabiri na kuelewa ukubwa wa janga la corona, wameelekeza lawama zao kwa China kama njia ya kupotosha fikra za walio wengi huko Marekani na duniani kiujumla. Trump na waziri wake wa mambo ya nje, Mike Pompeo, wanadai kuwa China haikuwa muwazi kuhusu ukubwa wa janga la corona na haikutoa taarifa kamili kwa taasisi za kimataifa. Hivi karibuni wabunge wa chama cha Republican waliwasilisha mpango unaodai kuwa China haikuwajibika ipasavyo katika vita dhidi ya corona na walidai iliruhusu ugonjwa huo uenee duniani na kutaka walipwe fidia. Hata hivyo mara chungu nzima China imekuwa ikikanusha madai hayo ya viongozi wa Marekani na kusisitiza kuwa, ilishirikiana kikamilifu na taasisi za kimataifa katika jambo hilo, isipokuwa tu serikali ya Marekani ambayo imefeli kukabiliana na ugonjwa huo, inatafuta kila njia kujipapatua na lawama. Duru mbalimbali duniani zimekuwa zikiilaumu Marekani kwa kutoa madai yasiyo na msingi kuhusu ugonjwa wa COVID-19 baada ya yenyewe kufanya uzembe na kushindwa kukabiliana nao. 

Kwa kweli tuhuma zinazotolewa na Donald Trump kuhusu corona na vitisho vyake dhidi ya China ni muendelezo wa siasa zake za chuki dhidi ya Beijing kwani Washington inaiona China ni mpinzani wake mkubwa duniani katika kila upande; kiuchumi, kiteknolojia, kiushawishi n.k. Hata hivyo kama tulivyotangulia kusema, takriban hakuna yeyote duniani anayekubaliana na tuhuma hizo za Marekani dhidi ya China kuhusu corona, si Shirika la Afya Duniani (WHO) na wala si taasisi nyinginezo za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa.