Rais Yoweri Museveni ametangaza kuwa kuvaa barakoa ni jambo la lazima nchini humo kuanzia leo katika kipindi hiki ambacho marufuku ya kutotoka nje imelegezwa kidogo.

Hatua hiyo ilitangazwa jana Jumatatu usiku ambapo rais Museveni alihutubia taifa baada ya kumaliza siku 35 za marufuku ya kutotoka nje ama 'lockdown'.

Museveni amesema watu wanaweza kuvaa barakoa ambazo zimeshonwa kienyeji na vitambaa.

Katika hatua nyingine, Museveni amesema kuwa kuruhusu shughuli kuendelea kama awali inabidi kufanyike kwa umakini na mpangilio ili kuzuia virusi kusambaa kwa kasi.

Kwa kuanzia, ameruhusu maduka ya jumla, karakana za kukarabati magari, maghala kufunguliwa. Pia ameruhusu wafanyakazi wa bima na idadi ndogo ya wanasheria kurejea kazini.

Masharti mengine yaliyosalia ya marufuku ya awali bado yanaendelea mathalani kufungwa kwa mipaka ya nchi, kutoruhusu usafiri binafsi na wa umma, mikusanyiko ya watu na marufuku ya kutotoka nje usiku bado yangalipo kwa kipindi kingine cha siku 14.

Museveni amesema hatua hizo mpaka sasa zimetoa mafanikio ambayo ni kuzuia kusambaa kwa kasi kwa virusi hivyo.
 
Idadi mpya ya maambukizi kufikia leo asubuhi nchini humo imeongezeka kutoka 89 mpaka 97.

Kati ya wagonjwa hao, Waganda ni 57. Mpaka kufikia Jumatatu, madereva 30 wa malori walikuwa wamekutwa na corona nchini humo, kati yao Wakenya 13 na Watanzania 12.