Tanzania inaungana na dunia nzima katika kuadhimisha sherehe ya Uanuwai wa Utamaduni ambazo hufanyika kila mwaka tarehe 21 Mei. Katika sherehe za mwaka huu wa 2020, kila mwanajamii kwa nafasi yake na katika eneo lake aendelee kuchukua tahadhali zinazoendelea kutolewa na Serikali juu ya kupambana na janga hili la ugonjwa wa Covid 19 nchini na kuendelea na shughuli za kiuchumi.
 
Tunajivunia na kuuenzi Uanuwai wa Utamaduni nchini kwa zaidi ya miaka 56 ya Uhuru ambapo uanuai wa Utamaduni wa jamii zaidi ya 120 umekuwa fursa ya kuleta amani, faraja, usawa na maendeleo kwa jamii ya Watanzania. Nina thubutu kusema Uanuwai wa Utamaduni ni sawa na mishipa ya damu kwenye mwili wa binadamu. 
 
Uanuwai wa utamaduni umeendelea kuwa ngao na kinga ya jamii dhidi ya majanga mbalimbali yanayolikumba Taifa na Dunia. Uanuwai huu, umejipambanua katika mila na desturi, sanaa, lugha na historia za jamii ya Tanzania. Kila mwanajamii amewajibika katika kutoa mchango wa maendeleo ya uanuwai wa utamaduni iwe kwa kuheshimu utamaduni wake kufanya kazi kwa bidii, kutunza amani ya nchi, kuheshimu vitambulisho na rasilimali za Taifa, sheria na taratibu zote zilizowekwa na Nchi.
 
Kutokana na juhudi hizi, Watanzania wamekuwa mstari wa mbele katika kulinda, kuendeleza na kuhifadhi anuwai wa kiutamaduni nchini hatua ambayo imeleta urahisi wa kukabiliana na janga la dunia la ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) kudhibitiwa kikamilifu. Viongozi wa Kitaifa, wasanii, wazee wa kimila na wazazi wametumia majukwaa mbalimbali kujadili na kuelimisha umma umuhimu wa kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
 
Natoa wito kwa Watanzania wote kutunza na kuendeleza Uanuwai wetu wa Utamaduni, kwani ukipotea hauna mbadala wake, tuzingatie kaulimbiu ya mwaka huu 2020 inayosema “Tulinde na Kudumisha Uanuwai wa Utamaduni Wetu, Kwa Kufanya Kazi kwa Bidii na Kuchukua Tahadhali dhidi ya Janga la Ugonjwa wa COVID-19”. 
 
Kwa niaba ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nawatakia maadhimisho mema.

Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb),
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO