Trump atangaza kufanya mkutano wa ana kwa ana na G7 katika makazi yake ya mapumziko
Rais wa Marekani Donald Trump amesema anaangazia kuitisha mkutano na wakuu wa kundi la mataifa saba yenye nguvu zaidi kiuchumi duniani, G7 katika makazi yake ya mapumziko ya Camp David, licha ya mzozo unaoendelea wa virusi vya corona.
Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter “kurejea kwenye hali nzuri” na kusema huenda ataitisha mkutano huo yeye mwenyewe mwezi Juni, badala ya kufanya kwa njia ya video kama ilivyopendekezwa awali.
Amesema mataifa wanachama pia yameanza kuimarika na hiyo ni ishara njema. Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema atasubiri aone kile kitakachotokea, huku rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema atahudhuria iwapo mazingira ya kiafya yataruhusu.
Wakati Trump akisema uwezekano huo ni ishara ya mambo kurejea katika hali ya kawaida, Brazil imeripoti idadi ya juu kabisa ya vifo, wakati janga hilo likiliathiri vibaya kabisa taifa hilo la Amerika ya Kusini.