Na Ismail Ngayonga-MAELEZO
SEKTA ya Kilimo nchini imeendelea kuwa ni Sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla hususan katika wakati huu tunapojizatiti kufikia uchumi wa viwanda.
 
Katika  kipindi  cha  miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia  bei  za  Mwaka  2015  limeongezeka  kwa asilimia 17 kutoka Tsh. Trilioni 25.2 Mwaka 2015 hadi Tsh. Trilioni 29.5 Mwaka 2019.
 
Vilevile, sekta imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58 Mwaka 2018 na kuchangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa huku sekta ndogo ya mazao ikichangia asilimia 16.2 na hiyo imetokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo vyakula vinavyotokana na mazao ya kilimo.
 
Ili kufikia kiwango malengo makubwa ya uzalishaji wa mazao, Sera zinazoongoza utafiti zina mchango mkubwa katika kupanga maendeleo ya sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na ya kuboreshea viwango vya maisha ya wananchi kwa kuchochea ukuaji na kuongeza tija katika sekta muhimu za uzalishaji za uchumi wa taifa.
 
Historia inaonyesha kuwa nchi zilizozingatia sera zenye mwelekeo wa utafiti thabiti zimefanikiwa kujenga uchumi wenye ushindani kwa kutumia rasilimali walizonazo, na kuziendeleza kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi wao.
 
Katika jitihada hizo, Serikali kupitia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imeendelea kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, misitu na uvuvi katika eneo la Tafiti na Ushauri elekezi ili kutoa huduma ya elimu ya ushauri wa kitaalamu kwa wakulima.
 
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/2021, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako anasema Serikali kupitia SUA imeendelea na miradi mipya 13 ya utafiti yenye lengo la kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, misitu na uvuvi  ili kuwezesha wananchi kuzalisha mali na malighafi za mazao ya kilimo kwa ajili ya viwanda.
 
Prof. Ndalichako anasema Chuo hicho pia kimeweza huduma ya elimu ya ushauri wa kitaalamu kwa wakulima 9,500 kwa kutumia vituo atamizi, mashamba darasa, semina, kozi fupi, runinga na redio kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija na kupunguza umaskini kwa wananchi.
 
‘Mafunzo hayo yametolewa kwa wakulima katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Iringa, Dodoma, Tabora, Tanga, Pwani na Morogoro kwa lengo la kutoa elimu kuhusu kilimo na ufugaji’’ anasema Prof. Ndalichako.
 
Aidha Prof. Ndalichako anasema SUA pia ) imepima jumla ya sampuli 1,553 zikiwemo sampuli za udongo 1,180, za mimea 297, za mbolea za viwandani 20, za samadi tisa (9) na sampuli za maji 47 kutoka kwa watafiti mashirika ya kilimo, Viwanda na Taasisi mbalimbali pamoja na wakulima binafsi.
 
Waziri Ndalichako anasema kuwa Serikali imeingia mikataba mipya 13 ya mahusiano na Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo wafanyakazi na wanafunzi katika kufanya tafiti za kisayansi na kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa wananchi.
 
Anazitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sophia kilichopo Japan; National Institute of Health - Korea; Foundation Pierre Fabre - France; Kunming Institute of Zoology,  Chinese Academy of Science; Silverlands Tanzania Limited - Iringa, Tanzania; College of Animal Science and Technology Nanjing Agricultural University - China; Agronomos Sin Fronteras Foundation (ASFF ) - Iringa Tanzania; University of Leeds – UK; na Wuhan University (WHU) – China.
 
Akifafanua zaidi Prof. Ndalichako anasema katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia Serikali imejenga jengo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,400 kwa wakati mmoja litakalokuwa na maabara nane zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 100 kila moja.
Prof. Ndalichako anasema Serikali pia imekamilisha ujenzi wa jengo la utafiti wa wanyama na wadudu kwa ufadhili wa mradi wa Eastern and Southern Africa Centers of Excellence for Innovative Rodent Pest Management and Biosensor Technology Development (ACE II, IRPM and BTD) na kuendelea na ukarabati wa madarasa likiwemo jengo la Hay Building kwa lengo la kuongeza nafasi za kufundishia na kujifunzia.
Mazao ya Kilimo ni malighafi muhimu sana katika viwanda, hivyo ni utafiti ni nguzo muhimu sana inayoweza kuleta kuleta ubunifu wa bidhaa, uboreshaji wa bidhaa, kuongeza ufanisi wa huduma, tija na ubora wa utendaji katika soko.

MWISHO