Na Felix Mwagara, MOHA, Dar.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha Mahabusu waliopo katika Magereza mbalimbali nchini wanaanza kufanya kazi kama ilivyokuwa kwa wafungwa.

Amesema mchakato huo ambao tayari umeanza, utakapo kamilika utaleta mapendekezo madhubuti ya jinsi gani ya kuwatumia mahabusu hao pamoja na wafungwa katika kufanya kazi za uzalishaji mali na kuhakikisha Jeshi hilo linajitegemea kikamilifu.

Akizungumza na Maafisa na Askari Magereza katika Magereza ya Segerea, Ukonga na Keko jijini Dar es Salaam, leo, kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya siku moja ya kusisitiza magereza yanajitegemea nchini, alisema ili binadamu ale lazima afanye kazi, na pia vitabu vitakatifu vinasisitiza hilo, hivyo mahabusu wanapaswa kufanya kazi kwa kuwa nao wanakula vyakula magerezani.

“Kuna mjadala mkubwa tunaendelea kuchakata kuhusu mahabusu waweze kufanya kazi, lakini lengo letu sio kuwafanyisha kazi za sulubu, au kazi zinazotweza utu wao, hapana, wao pamoja na wafungwa wana adhabu wanayoitumikia, tunataka kuwatumia katika kuzalisha, kwahiyo watafanya kazi kama watu wengine wanavyofanya kazi, hili naomba lieleweke,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa, “Mjadala unaendelea na tutakuja na majibu jinsi ya kuwatumia mahabusu na wafungwa, lakini tutakuja na majibu yenye mapendekezo tutashirikiana, lakini tunataka kuwatumia kwa nia njema ya kuzalisha, kama mnavyojua binadamu asipofanya kazi asile na imeandikwa katika vitabu vitakatifu, kama mtu umemfungia ndani alafu hafanyi kazi na anadai chakula na ajue kwamba asipofanya kazi hana haki ya kula, wewe umekuja ni mahabusu ili upeleke tonge hapa lazima uzalishe, huwezi kusema sifanyi kazi kwasababu ni mahabusu, hapana tutakulinda hata kwa bunduki utafanya kazi.”

Alisema lazima kuwepo na mtazamo mpana, mkubwa katika masuala ya kuzalisha na kujitegemea kwa Jeshi la Magereza, kwa ajili ya kuzalisha pamoja na kutatua matatizo mengine ndani ya Jeshi hilo ikiwemo kujenga nyumba, kulipa umeme pamoja na mahaitaji mbalimbali ya Jeshi hilo.

“Kama nilivyosema mjadala bado ni mkubwa kwa wafungwa na tunafahamu wapo chini ya Magereza, lakini hao wengine tumepewa tuwatunze wapo chini ya vyombo vingine, hivyo tunaendelea na mchakato wa kujadiliana kuhusu hilo, na ukikamilika tutawaletea majibu,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa, dhana ya Jeshi hilo kuzalisha na kujitegemea ni agizo la Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dkt. John Magufuli kulitaka jeshi hilo kuzalisha kwa wingi ili kujitosheleza na kujitegemea.

Aidha, alilitaka Jeshi hilo kuhakikisha Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam yaanze kufanya kilimo cha mboga za majani na matunda pamoja na ubunifu wa uzalishaji mwingine katika mkoa huo, na magereza yaliyopo mikoani yaendelee na kilimo cha mpunga, mahindi, ufugaji pamoja na uzalishaji wa aina nyingine wanaoendelea nao katika maeneo yao.

Alisema kupitia uzalishaji mali huo utawezesha kupata fedha baada ya kuuza na kusaidia majukumu mengine ya Jeshi kuliko kutegemea fedha za matumizi mengine (OC) ambazo utolewa na Serikali kwa Jeshi hilo.

Pia Waziri Simbachawene amelitaka Jeshi hilo kuhakikisha wanahakiki mali zote za Jeshi ikiwemo mashamba yajulikane, na pia ijulikane yana hati au hayana, na mifugo ya Jeshi hilo ipo wapi na idadi yake ikiwa ni lengo la kutambua mali hizo na kuwekwa wazi kwasababu ni mali za umma.

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Solomon Urio, alimshukuru Waziri huyo kwa kufanya ziara katika Mkoa huo na kuwaomba viongozi mbalimbali nchini waweze kutembelea magereza ili waweze kujifunza na kujua kazi mbalimbali zinazofanywa na Jeshi mkoani humo.

“Tunakushukuru kwa kututembelea Mheshimiwa Waziri, na maelekezo uliyotaoa tutayafanyia kazi, na pia tunawaomba viongozi mbalimbali waweze kutembelea Magereza na kujua kazi mbalimbali tunazozifanya,” alisema ACP Urio.

Simbachawene amemaliza ziara yake ya siku moja kwa kutembelea magereza hayo, ambayo ni Gereza Kuu la Mahabusu Segerea, Gereza Kuu la Ukonga na Gereza la Mahabusu la Keko, ambapo katika ziara yake alipokua taarifa ya utendaji kazi kutoka kwa Wakuu wa Magereza hayo pamoja na kuahidi changamoto zao kufanyiwa.