Na Charles James, Dodoma
SERIKALI imetangaza kuvifuta rasmi vyama vya Ushirika 3,348 ambavyo vingi ni hewa huku ikisema zoezi la kufuta vyama hivyo litakua endelevu Kwa vyama vitakavyoshindwa kutekeleza majukumu ya kuanzishwa kwake.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Josephat Hasunga wakati akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma ambapo pamoja na kufuta vyama hivyo pia amevitaka vyama vilivyosalia kuimarisha mwenendo wao.

Vyama ambavyo vimefutwa ni Saccos 2,513, AMCOS 229, Mifugo 77, Vyama vya walaji 27, Vyama vya huduma 70, Vyama vya ufugaji Nyuki 15, Vyama vya wenye nyumba 9, Vyama vya Madini 22, Vyama vya wenye Viwanda 79, Vyama vya Uvuvi 32, Vyama vya Umwagiliaji 31 na vinginevyo 244.

Kabla ya kufutwa kwa vyama hivyo, Idadi ya vyama vya ushirika ilikua 11,626 hivyo baada ya kufutwa kwa vyama 3,348 sasa vyama hivyo vya ushirika vinabaki kuwa 8,611.

Waziri Hasunga amewataka wanachama na wakulima wanaotumia vyama vya ushirika nchini kufunga akaunti Benki ili mkulima kujihakikishia malipo yake.

Amesema kama wakulima wakifanya hivyo itakua ni mojawapo ya suluhu kwa udanganyifu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wasio waaminifu wakati wa malipo.

Akizungumzia mfumo wa ununuzi wa mazao Nchi nzima, Waziri Hasunga amesema njia pekee ya kumkomboa Mwananchi ni kupitia ushirika hivyo kuwataka wananchi wajiunge na vyama hivyo ili wanufaike na ushirika.

" Wananchi wakiuza Kwa pamoja ni rahisi kupata bei nzuri, hata hivyo kumetokea malalamiko mengi katika baadhi ya mikoa kuwa wananchi wananyanyasika sana na mfumo wa vyama vya ushirika na stakabadhi ghalani.

Sasa ili mfumo wa stakabadhi ghalani uweze kufanyika sawasawa naagiza kuwepo kwa chama cha msingi kilichosajiliwa katika kijiji husika, kuwepo kwa ghala lililosajiliwa na Bodi ya Maghala, kuwepo kwa mfumo wa kufanya minada kwa njia ya ushirika na kuwepo kwa wanunuzi wa kununua kwa minada," Amesema Waziri Hasunga.

Kutokana na changamoto hizo, Waziri Hasunga ameagiza kuhakikisha kuwa katika kila kijiji kunakua na soko la awali ambalo wananchi watauza mazao yao lakini pia kuwe na soko la upili ambalo wananchi, vyama vya ushirika na wafanyabiashara wa ndani wataruhusiwa kuuza mazao yao kwa wafanyabiashara wa nje.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Vyama vya Ushirika nchini Titus Kamani ameishukuru Serikali kwa namna ambavyo imekua ikizingatia maslahi mapana ya wananchi na kwa kusimamia vema uendeshaji wa vyama hivyo.

" Niipongeze sana serikali imekua mara zote ikiwajali sana wanachama wa Ushirika ambao wengi wao ni wananchi wanyonge na ndio maana tunaona mara kadhaa vyama hivi vinapoenda kinyume basi serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekua ikichukua hatua kali ikiwemo kuvifutia usajili vyama vinavyoenda kinyume na uanzishwaji wake," Amesema Kamani