WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imemwita Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk Imni Patterson (pichani), kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ambayo ubalozi huo umekuwa ukiyaandika katika mitandao yake ya kijamii bila ya uthibitisho.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wizara hiyo, Emmanuel Buhohela, Kaimu Balozi huyo amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge, kwenye ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.
Ilieleza kuwa katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu alieleza masikitiko yake kutokana na namna ambavyo ubalozi huo umekuwa ukitoa taarifa mbalimbali za ushauri wa kiusafiri zinazoandikwa na kusambazwa na Ubalozi wa Marekani kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo namna Tanzania inavyoshughulikia ugonjwa wa Covid-19.
Akitolea mfano, Katibu Mkuu alizitaja taarifa zilizotolewa na ubalozi huo Mei 13, 2020 na Mei 25, 2020 kwenye mtandao wa “Twitter” wa ubalozi huo ambazo zote zilionekana kukusudia kutoa tahadhari kwa raia wa Marekani waliopo nchini na wanaotarajia kuja Tanzania kuwa Jiji la Dar es Salaam siyo salama kutokana na kuwepo idadi kubwa ya wagojwa wa Covid-19.
“Tahadhari hizo pia zimeendelea kudai kuwa hospitali nyingi jijini Dar es Salaam (bila ya kuzitaja hospitali hizo) zimefurika wagonjwa wa Covid-19, jambo ambalo siyo kweli na lina uwezekano wa kusababisha taharuki kwa Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi ilhali hali halisi sivyo ndivyo inavyodaiwa,” ilieleza taarifa hiyo.
Ilisema Katibu Mkuu amemjulisha Kaimu Balozi kuhusu umuhimu wa ubalozi kutoa taarifa zilizothibitishwa hususani kwa sababu serikali haina kizuizi cha aina yoyote kwa mabalozi kutafuta na kupata taarifa sahihi na zenye ukweli.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amemshukuru Kaimu Balozi huyo kwa ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Marekani katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama na maeneo mengine ya maendeleo.
The post Serikali yamwita balozi wa Marekani kuhusu kauli za Covid-19 appeared first on Bongo5.com.