Mwandishi- EDDAZARIA G.MSULWA
Age-18+
Simu-0768516188

Kila mwanachuo ndoto zake ni kuweza kupata ajira nzuri sana kwa kile alicho kisomea kwa miaka mingi sana kipindi alipo kuwa chuoni. Ila mambo ni tofauti sana kwa kijana Evans Shika. Elimu ya Masters of Business Administration – International Business aliyo isoma katika chuo cha IFM, inamfanya azidi kutesaka sana katika swala zima la kutafuta ajira. Kila ofisi aliyo weza kupeleka maombi ya kuajiriwa, ana kataliwa na kujikuta ana zidi kukumbana na maisha magumu  sana yaliyopo katika jiji la Dar es Salaa.
“Evans”   
Lukas rafiki yake wa karibu alimuita huku akimtazama usoni mwake.
“Niambie kaka”   
“Nina mazungumzo muhimu nahitaji kuongea na wewe. Kmaa unaweza kunipatia muda wako basi nakuomba tuzungumze”
“Sawa kaka tuzungumze tu”
Evans alizungumza huku akikaa kitako kitandani na kumtazama Lukas aliye kalia stuli moja iliyomo ndani ya geto hilo.
“Lidya ni mjamzito na hapa ninavyo zungumza kwao wametambua hilo na baba yake ameamua kumfukuza”
“Mungu wangu….Sasa utafanya nini kaka?”
“Sina jinsi zaidi ya kumleta hapa kaka. Nilazima niishi naye kwa maana hakuna namna”
“Mmmm kaka sasa kweli tutaweza kuishi watatu geto moja!?”
“Ahaa kaka hatutaweza. Mimi naona kwa sasa uweze kujitafutia maisha mengine ndugu yangu. Usinifikirie vibaya au kuhisi kwamba nina kufukuza nyumbani kwangu. Hapana, ila shemeji yako ndio huyo ana kuja na kwakweli sikujipanga kabisa kuhimili maisha ya kuhudumia watu wawili.”
 
Maneno ya Lukas yakamstua sana Evans. Mapigo yake ya moyo yakaanza kumuenda kasi huku kijasho kikianza kumtiririka usoni mwake. Hakika toka alipo maliza chuo na kukosa ile mikopo ambayo wanapatia kwa ajili ya kujikimu, maisha yake yamekuwa magumu sana, kiasi cha kujikuta akipata hifadhi kwa rafiki yake Lucas ambaye naye kwa sasa amekabiliwa na majukumu mazito sana.
 
“Kaka wewe ni mwanaume. Ninakushauri, hembu jishikize kwenye vibarua vidogo vidogo japo upate vimiambili mia tatu vya kukukimu. Haya maisha ya kusema utafute kazi hizi ambazo mwisho wa siku unatoka hola, huoni kwamba una jicheleweshea malengo yako?”
 
Maneno ya Lucas hayakuweza kuleta matumaini wala faraja kwa Evan ambaye hatambui ni wapi atakapo kwenda. Kila akijaribu kulichanganua hili jiji la Dar es Salaam, hakika hana ndugu wa kuweza kuishi kwake.
“Evans, Evans”
“Naam kaka”
“Sijui umenielewa nilicho kuambia?”
“Yaa nimekuelewa kaka”
“Kuna ishu nyingi sana hapa mjini. Tazama mimi, ninaosha magari japo elimu yangu ni form four ila kidogo nina pata mia mbili mia tatu bro. Changamka hapa ni mjini usiamini sana kwenye maswala ya vyeti kaka.”
 
Evan taratibu akanyanyuka kitandani, akachukua begi lake la nguo pamoja na begi lake la mgongoni. Akafungua begi la mgongoni na kuhakikisha kwamba bahasha yenye vyeti vyake ipo salama. Alipo jiridhisha akalifunga na akalivaa mgongoni na kumtazama Lukas.
 
“Nashukuru kaka kwa kipindi chote ulicho weza kunivumilia kwa kukaa humu ndani. Nitaufanyia kazi ushauri wako”
“Nashukuru sana kaka. Kamata hii buku tano itakusaidia japo hata kwa chakula cha mchana huu na usiku”
Evans akautazaama mkono wa kulia wa Lukas unao mpatia kiasi hicho cha pesa. Kisha taratibu akaipokea na kuiweka mfukoni mwake.
“Asante kaka”
“Poa kaka ila nakuomba usinifikirie vibaya”
“Wala usiogope kaka, nimekuelewa na ninaelewa hali uliyo nayo ndugu yangu”
“Nashukuru sana kwa kuweza kulitambua hilo”
 
Lukas akanyanyuka kisha wakakumbatiana. Evans akatoka ndani ya chumba hichi. Akasimama eneo la nje la chumba hichi, akayatazama mazingira ya nyumba hii iliyopo, Tandale kwa tumbo. Taratibu akaanza kukatiza kwenye vichochoro vya nyumba hizi huku kichwani mwake akiwa na mawazo lukuki. Kila anavyo jaribu kumfikiria mama yake na mdogo wake wa kike walipo mkoni Kigoma, anashindwa kabisa kupata ujasiri wa kurudi kwao, kwani ufukara wa nyumbani kwao ndio umemfanya aweze kusoma kwa juhudi ili kujikomboa kwenye umasikini huo.
“Siwezi kurudi Kigoma”
 
Evans alizungumza mwenyewe huku akiendelea kukatiza kwenye vichochoro vilivyo jaa maji machafu, hii ni kutokana na mvua zinazo endelea kunyesha kwenye jiji la Dar es Salaam. Evans akiwa katika chochoro moja, ghafla akakutana na kundi kubwa la wahuni likiwa limebananisha dada mmoja aliye shika deli lililo jaa maandazi.
 
“Jamani maandazi yangu hayo ninauza musiyafanye hivyo”
Dada huyu alilalama huku akiwa amebananishwa ukutani, huku wahuni wengine wakiendelea kuyatafuna maandazi hayo bila hata ya kumuonea huruma.
“Tulia wewe. Kama hutaki tuyale tutakupa kifi** ambacho hujawahi kukipata toka uzaliwe”
Muhini mmoja alizungumza huku akimnyooshea panga la usoni dada huyo.
 
“Wewe mseng** una kodoa kodoa nini macho au unataka na wewe tuje kukupak** hapo”
 
Muhuni mwengine alizungumza huku akimnyooshea Evans kisu. Katika maisha yake yote Evans amekuwa ni mtu ambaye hapendelei kushuhudia mwanamke ana nyanyasika mbele ya macho yake. 

Kushikwa shikwa kwa dada huyu, kukazirudisha kumbukumbu zake miaka kumi na mbili iliyo pita, kipindi akiwa na miaka kumi na mbili. Marehemu baba yake, alikuwa akimtesa sana mama yake na kumpa kipigo kizito mithili ya mwizi. 

Mzee Shika alisifika kwa ulevi na ubabe katika kijiji chao. Alikuwa ni mtu mwenye roho katili sana asiye jali utu wa mtu mwengine. Si mama yake tu aliye kuwa akishushiwa kipigo bali hata yeye mwenyewe alikuwa akibamizwa kisaswa sawa. Chuki na hasira juu ya mateso anayo yapata mama yake, yakatengeneza tabaka baya sana moyoni mwa Evans dhidi ya baba yake.
 
Usiku wa siku moja kama kawaida, baba yake alirudi akiwa amelewa chakari. Kitendo cha mke wake kuchelewa kumfungulia mlango, ikawa ni kosa kubwa sana kwake. Alimkamata mke wake na kuanza kumpiga bila ya huruma, huku mama Evans tumboni mwake akiwa ni mjamzito. Vilio vya mama yake akiomba msaada kwa watu vikamfanya Evans, kuvuta shoka alilo liweka chini ya kitanda chake na kutoka chumbani kwake huku akiwana hasira sana. Akaelekea kilipo chumba cha mama yake. 

Kwabahati nzuri akakuta chumba cha wazazi wake kikiwa wazi. Akaingia ndani na kumkuta mama yake akiwa amelala sakafuni huku akiendelea kushindiliwa mangumi ya uso na mzee Shika. 
 
Shetani wa hasira na ujasiri, akamjaa Evans moyoni mwake. Akanyanyua kishoka hicho na kumpiga nacho baba yake usogoni na kikazama karibia nusu, na kusababisha damu nyingi sana kuanza kutapakaa ndani ya chumba hicho.
“Evan..s mwanangu umeniua”
Mzee Shika alizungumza huku akianguka chini na kupoteza uhai wake hapo hapo. Kofi zito alilo pigwa dada huyo muuza maandazi likamtoa Evans kwenye dimbwi zima la mawazo. Akashuhudia jinsi wahuni hao wanavyo mchania nguo dada huyo huku wengine wakimshika shika maeneo ya siri pamoja na maziwa yake.
 
“MUACHENIII NIMESEMA”
Evans alizungumza kwa ujasiri na sauti ya juu. Wahuni hao wapatao sita, wakamtazama kwa sekunde kadhaa, kisha wakaanza kuangua kicheko cha dharau na kejeli.
“Mchekini huyu matak** ametokea wapi?”
 
Muhini mmoja alizungumza huku akianza kumsogelea Evans. Taratibu Evans akaweka begi lake chini na kujiandaa kwa lolote ambalo linaweza kujitokeza. Muhuni huyu aliye shika kisu mkononi mwake, akamvamia Evans, ila Evnas, hakuwa mjinga wala mzembe. Akamtandika ngumi nzito ya kichwa na kumfanya jamaa huyu kupepesuka na kuanguka chini. Wezake wakajawa na hasira na wakagairi zoezi la kumbaka mwanamke huyo. Wakamvamia Evans kwa pamoja na kuanza kupambaba naye. Wingi wao ukamfanya Evans ashindwe kabisa kuwakabili, wakamtembezea kichapo huku mmoja wao akimkita kisu cha tumboni na kumfanya Evans kuanguka chini.
 
“Oya mwana umeua. Msala msala huu.”
Mmoja wao alizungumza mara baada ya damu nyingi zilizo toka tumboni mwa Evans kumrukia mwilini mwake. Wakanza kuchanguka huku wakibeba mabegi yake yote mawili ya Evans, wakiamini kwamba ndani ya mabegi hayo wana weza kupata chochote kitu.
 
Mwanadada huyo akaanza kupiga kelele za kuomba msaada kwa watu kwani Evans anaendelea kutokwa na damu nyingi sana mwilini mwake. Wasamaria wema wakajitokeza na kuanza harakati za kumpa msaada Evans ambaye tayari amepoteza fahamu zake. Evans akafikishwa kwenye hospitali ya mwananyamala.
“Amefanyaje?”
Nesi mmoja aliuliza huku akiwatazama watu hawa alio mleta hapa hospitalini.
“Amevamiwa na wahuni”
Dada muuza maandazi alijibu huku jasho na machozi yakimwagika.
“Muna pf3 ya askari?”
“Hatuna dada, tunaomba mutusaidie”
“Sasa hatuwezi kumtibu mgonjwa aliye vamiwa bila ya kibali kutoka polisi. Akitufia hapa hamuoni kwamba itakuwa ni hatari kwetu.”
“Dada nipo chini ya miguu yako nakuomba mumpokee. Nipo tayari kwenda kuitafuta hiyo sijui pp3 polisi. Ila nakuomba mumtibu huyu kijana”
Dada muuza maandazi alizungumza huku akimpigia nesi huyu magoti. Ushawishi wa watu wengine walio msaidia Evans, ukaulainisha msimamo wa nesi huyu na kujikuta akikubaliana nao na kuwaomba wahakikishe kwamba wana tafuta kibali cha matibabu kutoka polisi.
 
“Nashukuru nashukuru sana dada”
Dada muuza maandazi alizungumza huku akitoka baru ndani ya hospitali hii na kuelekea kituo cha polisi. Akafanikiwa kufika polisi na kuelezea hali nzima ya tukio lilivyo tokea.
“Mgonjwa yupo wapi?”
Afande Mwahila aliuliza huku akimtazama dada huyu.
“Mwanayamala hospital”
“Unaitwa nani dada?”
“Naitwa Magreth”
“Hao vijana walitumia silaha gani kuwashambulia?”
“Visu na mapanga”
“Hao ni panya road. Wanarudi tena ehee?”
Askari mwengine alizungumza huku akimtazama Magreth usoni mwake. Magreth hakuweza kujibu jambo lolote zaidi ya kukaa kimya. Akaandikiwa ruhusa hiyo na kurudi hospitali ya Mwananyamala. Akamkabidhi nesi hati hiyo na matibabu ya Evans yakazidi kuendelea.
 
“Sasa mgonjwa amepoteza damu ya kutosha. Benk yetu ya damu hapa hospitalini ime kwisha. Kama unaweza kumchangia japo chupa moja itakuwa ni vizuri sana kwani kwa sasa mgonjwa yupo kwenye chumba cha upasuaji”
“Nipo tayari nesi”
 
“Basi jaza hii fomu hapa majina yako matatu. Kisha nifwate”
Magreth akasoma fomu hiyo ya kuchangia damu. Alipo ridhishwa na maelezo yaliyo andikwa kwenye fumo hiyo akajaza kilicho hitajika kisha akafwatana na nesi hiyo. Magreth akapimwa HIV na kwa bahati nzuri akakutwa yupo salama.
“Sasa unaweza kuchangia damu”
Nesi huyo alizungumza huku akianza taratibu za kutoa kiasi cha damu mwilini mwa Magerth.
“Ila mgonjwa atapona ehee?”
“Tuombe Mungu kwani kwa sasa yupo kwenye chumba cha upasuaji, madaktari wandelea na kazi ya kumuhudumia.”
“Ehee jehova, shusha muujiza wako mgonjwa aweze kupona. Damu ya Yesu kristo ikamuangazie”
Magreth alijikuta akipiga maombi na kumfanya nesi huyu kumshangaa.
“Mgonjwa ni nani yako?”
“Ni mpita njia”
“Mpita njia tu ndio una muombea hivyo. Mimi nilidhani ni kaka yako au ndugu yako kumbe mpita njia?”
Maneno ya nesi huyu yakauumiza moyo wa Magreth, ila hakuhitaji kumjibu chochote zaidi ya kuendelea kumlilia na kumuomba Mungu wake kimoyo moyo.
 
Madaktari wakazidi kujitahidi kwamba wana fanya upasuaji wa kukitoa kisu alicho chomwa Evans tumboni mwake. Upasuaji huo ukafanikiwa kuisha salama ndani ya masaa mawili. Evans akapelekwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi huku akiwa hajitambui kabisa.
“Nina weza kumuona mgonjwa wangu dokta?”
Magreth aliuliza swali huku akiwa amesimama nje ya chumba cha wagonjwa mahututi.
“Hapana kwa sasa huwezi kumuona kwani hali yake haijawa sawa”
“Ila anaweza kupona?”
“Hilo ni jambo la kumuomba Mungu, ila kwa sisi tumeweza kuikamilisha kazi yetu. Hatua inayo fwata ni hatua ya Mungu”
Dokta Mkama alimjibu Magreth kwa sauti ya upole huku akimtazama usoni mwake.
“Nashukuru”
“Nifwate ofisini kwangu”
Dokta Mkama na Magreth wakaongozana hadi ofisini na wakaka kwenye viti vilivyomo ofisini humo..
“Mgonjwa wako ana itwa nani?”
Magreth akaka kimya huku akimtazama dokta Mkama.
“Mbona kimya”
“Ahaa…simfahamu mgonjwa”
“Humjui? Mbona ume muhangaikia kwa kiasi kikubwa sana ikiwa mtu umtambui?”
“Bila ya huyu kaka mimi sasa hivi wala nisinge kuwa nimekaa mbele yako na kujibu maswali unayo niuliza. Alijitolea kupamabana na kundi la wahuni wa Panya Road, ili kuweza kuyaokoa maisha yangu.”
Magreth alizungumza huku machozi yakimwagika usoni mwake.
“Okay nimekuelewa. Je upo tayari kubeba gharama za kutibiwa kwa mgonjwa au kuna namna nyingine labda ya kuwasiliana na ndugu zake, wakakusaidia?”
 
Magreth akakaa kimya huku akitafakari. Kwaufupi maisha yake naye ni magumu sana, biashara ya kutembeza maandazi mtaani ndio inayo mfanya aweze kuishi katika jiji hili la Dar es Salaam. Japo na uzuri wa kipekee alio barikiwa na Mungu, ila haitaji kuutumia uzuri wake huo kuwa kigezo cha kujipatia kipato kwa njia ya umalaya wa kujiuza.
“Nakusikiliza upo tayari tukuandike wewe ndio msimamizi wa mgonjwa huyu”
Magreth akamtazama daktari Mkama kisha akamuitikia kwa kutingisha kichwa, akimaanisha kwamba ame kubaliana nahilo.
“Sawa nitakuandikia gharama zote hapa ambazo tumeweze kuzitumia katika kumuhudumia mgonjwa wako. Na tutakupigia bei ya yeye kulala ICU kwa siku moja”
“Sawa dokta”
Magreth akakaa kimya huku akimtazama dokta Mkama jinsi anavyo endelea kucharaza kwa peni karatasi iliyopo mezani mwake. 

Dokta Mkama alivyo maliza kuiandika karatasi hiyo, akaipitia kwa kuisoma kama kila alicho kiandika ni sahihi kisha akamkabishi Magreth. Taratibu Magreth akatupia macho yake kwenye karatasi hiyo. Moyo ukampasuka, kwani gharama iliyo andikwa kwenye karatasi hiyo ni kubwa na toka kuzaliwa kwake hajawahi kumiliki kiasi hicho cha pesa .
                                                                                                   ITAENDELEA
Haya sasa mambo ndio yameanza? Evans hali yake ni tete kitandani. Msaada wake wa mwisho ni Magreth ambaye naye uwezo wake ni duni, je ni wapi Magreth atakapo weza kupata kiasi hicho kikubwa cha pesa? Endelea kufatilia kisa hiki cha kusisimua, usikose sehemu ya 02