Maafisa nchini katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Rivers nchini Nigeria wamevunja hoteli mbili kufuatia madai ya kukiuka sheria za kukaa nyumbani zilizowekwa kwa lengo la kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.
Gavana wa jimbo hilo Nyesom Wike, ambaye alisimulia kuvunjwa kwa Hoteli ya Edemete Hotel na Prodest Home Jumapili, alisema kuwa waliofanya shughuli hiyo walikuka maagizo kwamba hoteli zinapaswa kufungwa.
Alisema kuwa watu waliopatikana na virusi vya corona walipatikana katika hoteli mbali mbali katika jimbo hilo. Lakini hakusema iwapo yeyote ambaye ana maambukizi ya Covid-19 amekuwa akiishi katika hoteli hizo mbili zilizovunjwa.
‘Tulikataa kutoa hongo’
Mameneja wa hoteli zote mbili wamekamatwa, lakini mmiliki wa Prodest Home amekana kwamba hoteli yake ilikua imefunguliwa.
“Hoteli haikua ikifanya kazi na 70% ya wahudumu walikua wamerudishwa nyumbani ,” Gogorobari Promise Needam alisema.
“Kulikua na watu watatu tu katika hoteli.
“[Maafisa ] walikuja na walikua wakiomba rushwa wakasema watatuacha tuendelee kufanya kazi, kama tutawapatia pesa lakini tukawambia hatufanyi kazi kwa hiyo hatuna pesa za kuwapatia ,” alisema .
Serikali ya jimbo la Rivers amekanusha shutuma hizo.
Jimbo hilo kwa sasa lina jumla ya visa 15 vya maambukizi ya virusi vya corona na imerekodi vifo viwili.
Amri ya kukaa nyumbani iliwekwa katika mji mkuu wa jimbo hilo, Port Harcourt, Alhamisi iliyopita.
Nigeria ina zaidi ya visa 4,300 vilivyothibitishwa vya virusi vya corona, huku mji mkuu wa biashara wa Lagos ukiwa ni kitovu cha maambukizi.
Lakini sharia ya kukaa nyumbani ambayo iliwekwa huko, na katika baadhi ya majimbo mengine, mwezi Machi ililegezwa.
Wataalamu wa sheria wamesema kuwa hatua zilizochukuliwa katika Rivers na gavana wa jimbo zinaweza kupingwa mahakamani.
Sheria kali ya kukaa nyumbani
Lakini serikali ya jimbo inasema kuwa Bwana Wike alisaini sheria ya kumpa mamlaka ya kutekeleza amri ya kukaa nyumbani.
Jimbo hilo limekua likikosolewa kwa kuweka sheria kali za kukaa nyumbani, ambazo zinaamuru masoko, na maeneo ya kuuza chakula kufungwa.
Madaktari, mafamasia na wafanyakazi wengine wa kazi muhimu pia wameripoti kuwa wamekua wakinyanyaswana wakati mwingine kukamatwa kwa kukiuka sheria ya kukaa nyumbani.
Maafisa wameweka vizuizi katika barabara kuu katika mpaka wake wa mashariki ili kuimarisha marufuku ya usafiri baina ya majimbo ,wakiwashutumu maafisa wa usalama kwa kuwaibia watu nyakati za usiku.
Maafisa pia wanapanga kufanya mnada wa kuuza magari yaliyokamatwa kutoka kwa wale wanaokiuka amri ya kukaa nyumbani.
Ni wale tu waliopokea vibali maalumu, vilivyotolewa na gavana mwenyewe wanaoruhusiwa kutembea.
Lakini, inaonekana wale waliomo katika serikali pekee ndio wenye waraka unaoelezea ni vipengele gani hasa kwani wakazi wa jimbo hilo wameiambia BBC kuwa hawaielewi.
Maafisa wa jimbo hilo hawakujibu BBC walipoombwa kuwasilisha nakala ya sheria hiyo.
‘Matumizi mabaya ya ofisi ‘
Wakili Ahmed Abass aliiambia BBC kwamba sheria hiyo ya gavana haiwezi kumpa mamlaka ya kuvunja jengo.
“Sheria ya amri huundwa na rais au gavana kwa kuzingatia sheria zilizopo nchini,” alisema na kuongeza kuwa haiwezi kwenda zaidi ya katiba, ambayo inatoa fursa ya kesi huru.
“Kile ambacho [Bwana Mike] alipaswa kufanya ni kuwakamata wamiliki wa hoteli, awapeleke mahakamani na wangeshitakiwa ,” aliiambia BBC.
Alielezea matendo ya gavana kama “utendaji wa kizembe na matumizi mabaya ya ofisi “.
Nigeria ina mfumo wa utawala wa shirikisho na majimbo hubuni sheria fulani kwa ajili ya masuala yanayoyahusu.
Bwana Wike binafsi alizunguka binafsi katika siku za mwanzo za amri ya kukaa nyumbani kufuatilia iwapo sheria hiyo inatekelezwa na akasema kuwa aliridhika jinsi watu wanavyoheshimu maagizo wanayopewa.
Katika tukio moja, alichukuliwa picha ya video akiamuru kukamatwa kwa watu wawili barabarani na akaagiza wapelekwe mara moja kwenye kituo cha kujitenga.
Katika video nyingine alisema kuwa wahudumu wa afya wanatumia vibaya fursa yao ya kuwa wafanyakazi muhimu, akiwashutumu madaktari wanaume kwa kutumia fursa hiyo kuwatembelea wapenzi wao wa kike.
Zaidi ya watu 200 walikamatwa katika siku ya kwanza ya amri ya kukaa nyumbani na kupelekwa kwenye kituo cha kujitenga .
Mahakama hatimae iliwapata na hatia 170 miongoni mwao na kuwalipisha faini ya dola 128.
Mwandishi wa BBC Karina Igonikon aliyeko Port Harcourt anasema kuwa watu wamekua wakihangaika kutokana na sheria za kukaa nyumbani na hilo huenda linaweza kuwa lilishawishi uamuzi wa gavana wa kulegeza sheria hizo siku ya Jumapili.
Gavana alitangaza kuwa watu wanaruhusiwa kutoka nje Jumanne na Jumatano wiki hii ili kupata hewa safi ya kupumua” na kununua bidhaa.
The post NIGERIA: Hotel zavunjwa na kuharibiwa ili kudhibiti maambukizi ya Corona appeared first on Bongo5.com.