Na Ismail Ngayonga, MAELEZO
SERIKALI ikishirikiana na wadau mbalimbali kutoka Sekta Binafsi imekuwa ikitekeleza majukumu mbalimbali ya kuwawezesha Wananchi Kiuchumi ili  kumuwezesha Mtanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kumiliki rasilimali.


Ili kuweka msisitizo zaidi katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, Serikali ilitunga Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 yenye lengo la kutoa mwongozo wa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata fursa za kiuchumi na kuwawezesha kuwa na kauli na ushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lilianzishwa kupitia sheria ya Taifa ya uwezeshaji wananchi Kiuchumi  namba 16 ya mwaka 2004, ikiwa ni chombo cha juu cha kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Aidha, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ambalo lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, linasimamia  mkakati wa Kitaifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kupitia madawati ya uwezeshaji kuanzia ngazi ya Wizara , Idara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri zote nchini.uchumi.

Katika kukabiliana na tatizo la mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini, Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria na Miongozo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kukuza ajira na kipato kwa wananchi.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/21, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo anasema hadi Februari 2020, mikopo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 25.38 sawa na asilimia 31.3 ya malengo ya mwaka wa fedha 2019/20 ilikuwa imetolewa kati ya lengo la kutoa mikopo ya Tsh. Bilioni 62.2.

Anasema mikopo hiyo ilitolewa kutokana na asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ambapo kati ya fedha hizo, Tsh. Bilioni 12.92 zimetolewa kwa vikundi 8,207 vya Wanawake, Tsh. Bilioni 9.54 zimetolewa kwa vikundi 4,266 vya Vijana na Tsh. Bilioni 2.91 zimetolewa kwa vikundi 915 vya Watu Wenye Ulemavu.

Akifafanua zaidi Waziri Jafo anasema katika kipindi cha miaka zaidi ya minne kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2020, Serikali imefanikiwa kutoa mikopo ya jumla ya Tsh. Bilioni 93.3 ambayo imenufaisha vikundi 32,553 vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ambapo mikopo hiyo imechangia kukuza uwekezaji mdogo na mkubwa na kuongeza kipato cha wananchi.

‘Kati ya mikopo hiyo,Tsh. Bilioni 54.08 zilitolewa kwa vikundi 20,542 vya Wanawake, Tsh. Bilioni 34.98 zilitolewa kwa vikundi 10,741 25 vya Vijana na Tsh. Bilioni 4.24 zilitolewa kwa vikundi 1,270 vya Watu Wenye Ulemavu na mikopo hiyo imewekezwa kwenye viwanda vidogo, kilimo na ufugaji wa kisasa, biashara, utunzaji wa mazingira, huduma za kifedha na huduma za usafiri.’’ anasema Waziri Jafo.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo anasema tayari baadhi ya Vikundi vimeanza kuwekeza katika  Wajasiriamali katika Halmashauri ya Mji Kahama ambapo ekari 500 zimetengwa na kuendelezwa ambapo tayari mradi huo umewezesha utoaji wa mikopo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 1.29 kwa vikundi 403 vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.

Aidha Waziri Jafo anaitaja miradi mingine kuwa ni pamoja na mradi wa Vijana wa kike wa ushonaji nguo katika Halmashauri ya Jiji la Tanga wenye gharama ya Tsh. milioni 100 na wanufaika 30, mradi wa kiwanda cha kuchakata kokoto katika Halmashauri ya Mji wa Makambako wenye uwekezaji wa zaidi ya Tsh. Milioni 45.

Miradi mingine ni pamoja na mradi wa ununuzi wa mashine ya kuchanganya malighafi wenye uwekezaji wa Tsh. Milioni 30.0 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, mradi wa kiwanda cha uchomeleaji cha Five Youth Innovators katika Halmashauri ya Manispaa 27 ya Ilemela wenye mtaji wa Tsh. milioni 20 na mradi wa usafirishaji katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke uliogharimu Tsh. Milioni 229. 32.

Waziri Jafo anasema Ofisi ya Rais-TAMISEMI pia ilifanikiwa kufuta malimbikizo ya fedha za mikopo ya miaka ya nyuma yaliyotokana na uwezeshaji wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vikundi vya Wanawake na Vijana kwa kuzingatia Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290.

Jitihada za kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi nchini ni jambo muhimu linalopaswa kuwa na mazingira wezeshi kwa Serikali kuhakikisha upatikanaji wa mitaji kwa kuimarisha na kuboresha vyanzo vya akiba sambamba na kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuwezesha mabenki kukopesha kikamilifu amana zilizopo na kwa gharama nafuu.