Mwanasayansi na mtaalam wa magonjwa nchini Marekani Anthony Fauci ameliambia bunge kuwa, kuna hatari kubwa ya maambukizi ya virusi vya Corona kurejea tena kwa nguvu iwapo majimbo mbalimnbali nchini humo yataanza kurejesha hali ya kawaida hivi karibuni.

Aidha ameonya kuwa hali ya kiuchumi huenda ikawa mbaya zaidi iwapo tahadhari hazitachukuliwa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Magonjwa ya kuambukia ameonya wabunge na maseneta kwamba hatua za kulegeza vizuizi vya kudhibiti ugonjwa Covid-19 zinaweza kusababisha hatari kubwa ya maambukizi ya virusi.

Onyo hilo linakuja wakati majimbo mengi yameanza kulegeza hatua za kudhibiti ugonjwa hatari wa Covid-19, bila kuheshimu maagizo yaliyotolewa na ikulu ya White House, ambayo yanapendekeza hasa siku kumi na nne za kupungua kwa janga hilo kabla ya kuondoa hatua za tahadhari.

Alipoulizwa kuhusu anachofikia baada ya majimbo mengi nchini Marekani kuchukuwa hatua ya kuanza kuondoa vizuizi vya kudhibiti ugonjwa wa Covid-19, amejibu: "Wasiwasi wangu ni kwamba majimbo, miji au mikoa hayafuati kabisa mapendekezo yetu, kwa sababu nadhani kama hii ikitokea kuna hatari kubwa ya maambukizi ya virusi vya Corona kurejea tena kwa nguvu, lakini pia hali ya kiuchumi huenda ikawa mbaya zaidi iwapo tahadhari hazitachukuliwa."

Wakati Marekani ikipitisha idadi ya watu 82,000 waliofariki dunia, Dk. Fauci ameonya, "Ongezeko la vifo itakuwa kubwa zaidi kuliko hiyo. Sijui ni kiasi gani, lakini nina uhakika kuwa idadi ya vifo itakuwa kubwa zaidi. "

Credit:RFI