Moto mkubwa ambao chanzo chake bado hakijafahamika umeibuka usiku wa kuamkia leo Jumamosi, Mei 23, 2020, katika Kisiwa cha Kome eneo la Mchangani, halmashauri ya Buchosa, Sengerema,  mkoani Mwanza na kuteketeza vibanda vingi vya wafanyabiashara pamoja na mali zilizokuwemo kwenye vibanda hivyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Muliro Jumanne Muliro, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo, madhara na thamani ya vitu vilivyoteketea.

Kwa mujibu wa mashuhuda,wamesema moto huo uliibuka majira ya saa 6 usiku na kudumu mpaka saa 10 alfajiri.

“Maduka, nyumba na vitu vingine vimeungua, watu wamepata hasara kubwa na wote bado wana taharuki kubwa kutokana na ajali hii. Imekuwa ni jambo la mara kwa mara kwa kisiwa hicho kukumbwa na matatizo  ya moto.

“Vibanda vingi ni vya muda, vimejengwa kwa mabanzi ya mbao na vipo karibu-karibu, kwa hiyo kikiwaka moto kimoja ni rahisi sana kuteketeza na nyingine kwa sababu mbao zenyewe zina mafuta,” amesema shuhuda mmoja

Baadhi ya mali nyingine zilitoteketea ni magari matano na samaki za wafanyabiashara.