Na John Walter-Babati, Manyara
Mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu amewaagiza maafisa biashara,maafisa tarafa na watendaji wa kata kufanya ukaguzi kwenye maduka ya jumla na reja reja na kuwawajibisha wanaouza sukari  tofauti na  maelekezo ya serikali.
 
Akizungumza katika baraza la madiwani la halmashauri ya mji wa Babati, Kitundu amesema bei ya sukari katika  mkoa wa Manyara kama ilivyoelekezwa ni shilingi laki moja na ishirini na nane (128,000)  kwa kilo hamsini ambayo ni sawa na shilingi 2,860 kwa kilo moja kwa bei ya jumla na shilingi 2,700 reja reja.
 
Mkuu wa wilaya amesema barua alioipokea kutoka kwa katibu tawala mkoa wa Manyara Missaile Musa inaelekeza kuwa mfanyabiashara yeyote asiuze sukari bei ya reja reja zaidi ya shilingi 2700 .
 
Amesema jambo la kusikitisha ni kwamba hata baada ya tangazo la serikali kutaka bei ishuke na matangazo kubandikwa katika maduka,baadhi ya wafanyabiashara mjini Babati bado wameendelea kukaidi na kuuza bei ya juu ya shilingi 3000 hadi 3500.
 
Amesema hawezi kukubaliana unyanyasaji huo kwa wananchi wakati serikali kupitia waziri mwenye dhamana na waziri mkuu walishatangaza kuwa hakuna uhaba wa Sukari nchini.
 
Ameeleza kuwa kukaidi maagizo ya serikali ni kosa kisheria hivyo watendaji  wa kata,vijiji na mitaa kuwachukulia hatua wote wanaokiuka.
 
Bodi ya sukari kupitia tangazo namba 284 lililotolewa Aprili 24,2020 chini ya sheria ya Sukari sura ya 251 ilitoa maekelezo ya bei ya sukari kwa jumla na reja reja kwa mikoa yote hapa nchini.