Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje walio tumia fedha za makusanyo ya ndani kiasi cha shilingi milioni 22.083 wametakiwa kuzirudisha ndani ya siku tatu huku Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa TAKUKURU ikielekezwa kusimamia hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ametoa agizo hilo  wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje la kujadili  hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Brig. Jen, Mwangela amesema hakuna mtumishi au mtu yeyote atakayetumia fedha za Serikali kwa Mkoa wa Songwe akabaki salama hivyo wote wanaodaiwa kukusanya mapato ya ndani na kuyatumia waziridishe au wakamatwe hadi watakapo zirudisha fedha hizo.

Amesema TAKUKURU hawapaswi kucheka na wala fedha za serikali kwakuwa madiwani wanahangaika kwa kushirikiana na serikali kubuni vyanzo vya mapato ili fedha hizo zitakazo kusanywa ziboreshe huduma za jamii na kukuza uchumi hvyo wanaozitumia hawapaswi kuvumiliwa.

Brig. Jen Mwangela ameongeza kuwa katika taarifa ya CAG Halmashauri ya Wilaya Ileje imepata hati yenye mashaka katika kuzingatia taratibu na sheria za manunuzi hivyo Mkurugenzi ahakikishe wataalamu wake wanafuata sheria na taratibu za Manunuzi pia madiwani wahahakishe wana simamia watumishi wasikiuke taratibu hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Haji Mnasi amemshukuru Mkuu Wa Mkoa wa Songwe kwa kushiriki kikao hicho na kuahidi kuwasimamia watumishi wafuate taratibu na sheria.