Mkutano wa Music In Africa wenye lengo la kudumisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kutumbuiza yaani (ACCES) unawaalika wanamuziki wa Kiafrika kutuma maombi yao kwaajili ya kushiriki kwenye mkutano huo wa ACCES 2020, utakaofanyika jijini Dar es salaam, kuanzia tarehe 26 hadi 28 Novemba mwaka huu. 

Mkurugenzi wa Music In Africa, Eddie Hatitye, anasema nafasi za upendeleo zitatolewa zaidi kwa bendi na wanamuziki wa Kitanzania kama washiriki wenyeji ili kuonesha ubora wa muziki wa Kitanzania na kubainisha kuwa mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 20/05/2020.

Mkutano huo wa ACCES, ambao umeandaliwa na Music In Africa Foundation (MIAF), hufanyika kila mwaka kwenye miji mbalimbali ndani ya Afrika, na kutoa fursa kwa wanamuziki kukuza na kujenge uwezo wao na kutumbuiza mbele ya hadhira iliyosheheni wageni wa kitaifa na kimataifa, ikiwemo waandaaji wa matamasha, mapromota, mawakala wa muziki, lebo za kurekodi muziki na hadhira yenye ushawishi mkubwa.

Mkutano huo pia unahusisha warsha mbalimbali za mafunzo, mazungumzo ya kitasnia, maelezo muhimu kupitia risala, maonesho ya moja kwa moja (mubashara), vikao vya kukuza umoja na mwasiliano, kurekodi nyimbo kwa pamoja na matembezi mbalimbali kwenye vituo muhimu vya tasnia ya muziki kwenye mji unapofanyika mkutano huo.

“ACCES inatoa nafasi za kushiriki kwa wanamuziki wanaoibuka wenye uwezo wa kutumbuiza moja kwa moja katika majukwaa na wenye utayari wa kutumbuiza katika majukwaa ya kimataifa. ACCES inahitaji washiriki walio tayari kunufaika kupitia mkutano huo kwa kukuza kazi zao kufikia hadhi za kimataifa” anasema Hatitye

Akizungumzia mlipuko wa unginjwa wa COVID 19, Hatitye anasema kuwa, wanafuatilia kwa ukaribu taarifa na kukagua maendeleo ya ugonjwa kwa nia ya kufanya uamuzi unaozingatia taarifa sahihi. 

“Kipaumbele cha kwanza cha Music In Africa Foundation ni usalama na ulinzi wa jamii yetu pana ya muziki na kila mtu anayehusika kutangaza tukio hili muhimu. Tunatumai kuwa ugonjwa wa COVID 19 utaisha mapema na mkutano wetu utaendelea kama ulivypangwa. Hivyo tunakuhimiza kuendelea kujisajili kwaajili ya mkutano na kutuma maombi ya kushiriki kwenye maonesho” anasema Hatitye.

Bonyeza hapa ili kupata Maelekezo ya namna ya kutuma maombi. Pia bonyeza hapa kupata Fomu ya maombi.