Meli ya kwanza ya mafuta kati ya tano zilizotumwa na Iran imewasili Venezuela, hii ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa ya ubalozi wa Iran nchini Venezuela, iliyotolewa kupitia mtandao wa twitter. 

Kwa pamoja meli hizo zinabeba mapipa ya mafuta yapatayo milioni 1.5, kama msaada kwa serikali ya Venezuela ambayo ni mshirika wa Iran. 

Nchi hizo mbili zinakabiliwa na vikwazo vikali vya Marekani. Venezuela ambayo pia ina utajiri mkubwa wa mafuta, inategemea msaada wa bidhaa hiyo kutokana na kuchakaa kwa viwanda vyake vya kusafisha mafuta. 

Kulikuwepo wasiwasi kuwa Marekani inaweza kuzizuia meli hizo baharini, na awali rais wa Iran Hassan Rouhani alikuwa ameonya kuwa ikiwa Marekani itazibugudhi meli hizo, Iran pia itazibugudhi meli za Marekani.

 Meli nne zilizoko njiani zinatarajiwa kuwasili mjini Caracas mnamo siku chache zijazo.