Chuo  Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimeanza usanifu wa kuunda mashine za kupumulia ya kiotomatiki inayowasaidia wagonjwa waliozidiwa kupumua na kufanya utafiti wa tiba mbadala zinazoonyesha uwezekano wa kuzuia au kupunguza makali ya ugonjwa wa corona.

Hayo yamo kwenye taarifa iliyotolewa  na Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Utafii), ikielezea mipango mbalimbali ambayo chuo kimejiwekea kusaidia jitihada za serikali kupambana na ugonjwa huo.

Ilisema UDSM pia imejiandaa kutoa fedha za utafiti kuhusu ugonjwa wa corona na imewahimiza watafiti wake kuendelea kufanya utafiti kwa kasi zaidi ili kupata tiba, kinga au njia nyingine ya kudhibiti maambukizo ya ugonjwa wa corona.

“Kupitia Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo-Utafiti, Chuo kimetenga fedha za utafiti na uvumbuzi kiasi cha Sh. 1,500,000,000 katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 kwa ajili ya mapendekezo yanayohusu athari za maradhi ya Covid-19 na mada nyingine za utafiti,” ilisema.

Ilisema UDSM, kupitia Kituo cha Maendeleo na Uhawilishaji wa Teknolojia (TDTC), kimebuni aina mbili za mashine za kunawia mikono za kiotomatiki na zinazotumia miguu.

Taarifa hiyo ilisema mashine hizo zina tangi la lita 250 na zimeandaliwa maalumu kwa ajili ya taasisi zinazohudumia idadi kubwa ya watu kama vile maeneo ya hospitali, viwanda na masoko.

Ilisema mashine hizo zinatoa sabuni ya maji na maji baada ya mtu kusogeza mikono karibu na sensa kwa upande wa mashine za kiotomatiki na kukanyaga pedeli kwa upande wa mashine zinazoendeshwa kwa kutumia miguu.

“Mashine hizi ni nzuri na hazihitaji kufunguliwa kwa mikono hivyo kupunguza uwezekano wa kuambukizana kwa kushika mabomba ya maji, aidha, Chuo tayari kimeshauza mashine hizi katika taasisi kadhaa zikiwamo, Amref, BoT, NHIF, TAA, WFP, TOL, Tamisemi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Tanesco,” ilisema taarifa hiyo.

Ilisema kama mchango wake kwa jamii, UDSM, kupitia TDTC, kinatengeneza mashine 20 za kunawia mikono zitakazotolewa kama msaada kwa hospitali za serikali zilizoandaliwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Covid-19 jijini Dar es Salaam na mashine zingine zitapelekwa katika vituo vikuu vya mabasi na daladala.

Ilisema kitengo cha vitambaa na nguo cha Idara ya Uhandisi Mitambo na Viwanda kikishirikiana na Kituo cha (TDTC) cha UDSM kimeanza uzalishaji wa barakoa za kiwango cha hali ya juu zenye matabaka matatu.

Kuhusu uzalishaji wa vitakasa mikono, ilisema UDSM imeanzisha mradi wa kuzalisha bidhaa hiyo kwa ajili ya matumizi yake ya ndani na ya umma kwa ujumla.

Ilisema taratibu za uzalishaji wa vipukusi hivyo vya mikono zimezingatia mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani, pamoja na viambata vingine, kunahitajika alkoholi isiyopungua asilimia 60.

Kuhusu upimaji wa ubora wa barakoa ilisema UDSM kupitia vitengo vyake mbalimbali kimekamilisha utafiti wa ubora wa barakoa za vitambaa zinazozalishwa na taasisi na watu mbalimbali.

“Matokeo ya utafiti huo utakaotolewa hivi karibuni yameainisha aina mbalimbali za vitambaa vinavyotumika na ubora wake na utafiti huo umekuja na mapendekezo ya namna ya kutengeneza barakoa za vitambaa zenye ubora,” ilisema.

Ilitaja hatua zingine inazochukua kuwa ni kubaini, kupima na kuchanganua sumu katika bidhaa asilia zilizoteuliwa kama vile matunda, mboga, mimea-tiba kwa ajili ya kuongeza virutubisho na kuandaa bidhaa za tibalishe.