Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwaamemwomba radhi Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kutokana na kauli za uongo alizowahi kuzitoa dhidi yake.

Katika nyakati tofauti, ndani na nje ya Bunge, Mchungaji Peter Msigwa aliwahi kutoa kauli za uzushi dhidi ya Kinana, akimtuhumu kujihusisha na ujangili na biashara ya nyara za serikali.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mbunge huyo alisema tuhuma zote alizowahi kuzitoa dhidi ya Kinana bungeni na kwenye mikutano ya kisiasa nje ya Bunge, hazikuwa na ukweli wala ushahidi wowote.

"Natoa tamko la kumuomba radhi Abdulrahman Kinana, ikumbukwe nilikuwa na kesi katika mahakama Kuu ya Tanzania iliyofunguliwa na Kinana kutokana na matamshi niliyowahi kuyatoa kumuhusisha na ujangili. Ninakiri tuhuma hizo hazikuwa za kweli, zilikuwa na malengo potofu

“Ni dhahiri kwamba nimemkosea, nimemdhalilisha na kumkashifu ndugu yangu Abdulrahman Kinana. Nimekutana na kuzungumza naye kuhusu jambo hili na kumwomba radhi. Ninashukuru kwamba amekubali kunisamehe.

“Bila shaka mtakubaliana nami kwamba Kinana ni mzalendo, muungwana na mstaarabu ambaye kwa kweli hastahili kukashifiwa wala kudhalilishwa.

"Nitaendelea kumheshimu kama alivyodhihirisha ustahimilivu na uungwana wake kwangu, kwa familia yangu na kwa Watanzania," Mchungaji Msigwa alisema.

Mahakama Kuu ya Tanzania, kupitia kesi namba 108 ya mwaka 2013, ilimkuta Mchungaji Msigwa na hatia ya kuandaa na kutoa kashfa dhidi ya Kinana kwa malengo ya kisiasa, kumchafulia jina na kumshushia hadhi yake katika jamii; ndani na nje ya nchi.

Kabla ya kupeleka suala hilo mahakamani, Kinana kupitia kwa Wakili wake, Erick Sikujua Ng’maryo, alimtaka Mchungaji Msigwa kufuta kauli zake hizo na kuomba radhi hadharani kwa kuwa hazikuwa na ukweli wowote. Mbunge huyo alikataa kufanya hivyo na kusema yuko tayari kujitetea mahakamani.