Serikali ya Rwanda imepunguza makali ya masharti iliyoweka kama hatua za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona tangu wiki sita zilizopita.
Tangazo hilo la serikali ambalo lilikuwa linasubiriwa sana linasema kuwa kuanzia Mei, 04 watu wataruhusiwa kurudi kwenye biashara zao binafsi na za umma huku kukiwa bado kuna masharti kidogo.
Mpaka sasa Rwanda imeripotiwa kuwa na wagonjwa wa corona 243 huku maambukizi mapya yakiwa ni watu 84 ambayo yaliripotiwa siku saba zilizopita ukilinganisha na visa 16 ambavyo viliripotiwa ndani ya siku saba zilizopita.
Waziri wa afya wa nchini humo anasema idadi hiyo ya maambukizi inaongezeka kwa sababu ya kuruhusu madereva wa maroli kuingia kutoka bandari ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania.
Hatua hizo ni zipi?
Shughuli za kibiashara za watu binafsi na umma zitarejea kuanzia tarehe 4, Mei, licha ya kwamba marufuku ya kutoka nje nchini humo itaendelea kuanzia saa mbili usiku mpaka saa kumi na moja alfajiri.
Masoko yatafunguliwa kwa wauzaji asilimia hamsini tu kuruhusiwa, shughuli za hoteli na migahawa zitarejea na kufungwa saa moja usiku.
Sehemu za michezo, mazoezi , vilabu vya pombe na sehemu za kuabudia zitabaki kuwa zimefungwa , hata hivyo mtu mmoja mmoja ataruhusiwa kucheza sehemu za wazi.
Usafiri wa umma unapaswa kuzingatia kutokaribiana kwa watu , lakini watu hawataruhusiwa kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.
Shule zote zitabaki zimefungwa mpaka mwezi Septemba 2020, na mipaka yote itabaki kuwa imefungwa isipokuwa mizigo ambayo inatakiwa kuingia nchini humo na raia wa Rwanda ambao wanataka kurejea nyumbani, tangazo hilo lilisema.
Rwanda lilikuwa taifa la kwanza la jangwa la sahara kuchukua hatua ya kupiga marufuku watu kutoka nje kabisa ikiwa ni jitihada za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Kwa upande wake Afrika Kusini leo Ijumaa imeanza kutekeleza masharti mapya yaliyowekwa na serikali baada ya wiki tano iliyowekwa na serikali kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona
Baadhi ya biashara zitaruhusiwa kufungua ikiwa ni pamoja na mikahawa ya chakula na familia kuruhusiwa kutoka majumbani mwao.
Serikali hata hivyo ita wapeleka maafisa zaidi was usalama kushika doria mitaani na ambao pia watahakikisha amri ya kutotoka nje nyakati za usiku inazingatiwa.
Uuzaji wa pombe bado umepigwa marufuku.
Afrika Kusini ni moja ya nchi za Afrika iliyoweka sheria kali ya kukabiliana na janga la corona.
Zaidi ya watu 100 wamethibitishwa kufariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 lakini amri ya kutotoka nje pia imeathiri pakubwa uchumi wa nchi hiyo.
Viwango vya umasikini viliripotiwa kupanda wakati wa marufuku ya kutotoka nje hali ambayo wadadisi wa masuala ya kijamii wanasema imepanua pengo kati ya matajiri na masikini.
The post Mataifa ya Afrika yaliyoanza kulegeza masharti ya Lockdown ya Corona appeared first on Bongo5.com.