Maafisa wanne wa polisi katika jimbo la Minnesota nchini Marekani wamefutwa kazi kufuatia kifo cha mtu mweusi ambaye alikuwa amekamatwa na kuonekana akizuiliwa chini kwa kushikwa shingo.

 

Afisa mkuu wa polisi katika jimbo hilo Medaria Arradondo amesema kwamba maafisa hao wanne sasa ”sio wafanyakzi wa kikosi hicho”.

Kanda ya video inaonesha, mtu huyo kwa jina George Floyd , akilia na kuwaambia maafisa hao weupe ”siwezi kupumua”.

Kisa hicho kinafanana na kile cha Eric Garner, mtu mweusi aliyefariki akikamatwa na polisi mjini New York mwaka 2014.

Shirika la ujasusi nchini Marekani FBi lilisema litachunguza kisa hicho cha Minneapolis kilichofanyika Jumatatu jioni.George Floyd

George Floyd aliwaambia polisi mara kadhaa kwamba hawezi kupumua

Maafisa wa polisi wa Minnesota walisema kwamba Floyd mwenye umri wa miaka 46 , ambaye alikuwa anafanya kazi kama afisa wa usalama katika mkahawa mmoja alifariki akifanyiwa matibabu kufuatia malumbano na maafisa wa polisi.

Siku ya Jumanne, Meya Jacob Frey alithibitisha kwamba maafisa hao wanne waliohusishwa na kisa hicho wamefutwa kazi. ”Huu ndio uamuzi tuliochukua”.

Katika mkutano na vyombo vya habari mapema, bwana Frey alikitaja kisa hicho kama cha kushangaza.

”Ninaamini kwamba kile nilichokiona ni kitendo cha makosa kwa kiwango chochote kile” , alisema.

”Kuwa mtu mweusi nchini Marekani hakustahili kuwa hukumu ya kifo”.

Ni madai ya hivi karubuni ya unyanyasaji unaotekelezwa na maafisa wa polisi dhidi ya Wamarekani weusi.

Visa maarufu vya hivi karibuni vinashirikisha afisa mmoja wa eneo la Maryland ambaye alimpiga risasi mtu mmoja akiwa ndani ya gari la kupiga doria.

Kisa hicho cha Minneapolis kilianza baada ya ripoti kwamba mteja mmoja alikuwa anajaribu kutumia noti bandia ya dola 20 katika duka moja.

Afisa huyo alimuona mshukiwa akiwa ndani ya gari lake, mtu huyo alikataa kukamatwa kulingana na maafisa wa polisi.

Waliambiwa kwamba mtu huyo ambaye hajatambulika alikuwa ameketi juu ya gari la rangi ya buluu na alionekana kana kwamba ametumia kishawishi fulani.

Waandamanaji wakimuombe George Floyd, ambaye kifo chake kimezua mjadala wa ukatili wa polisi Marekani

Waandamanaji wakimuombea George Floyd, ambaye kifo chake kimezua mjadala wa ukatili wa polisi Marekani

Baada ya kuagizwa kuondoka na kusimama kando ya gari hilo , jamaa huyo alikataa kukakamtwa lakini maafisa walifanikiwa kumfunga mikono yake kwa pingu na akaonekana kana kwamba alikuwa anaugua tatizo la tiba., taarifa hiyo iliongezea.

Katika kanda hiyo ya dakika 10 iliochukuliwa na shahidi , mtu huyo aliwekwa ardhini na afisa huyo na katika wakati mmoja alisikika akisema ”musiniue”.

Shahidi mmoja alisikika akimwambia afisa huyo kuondoa goti lake katika shingo ya mshukiwa huyo, akidai kwamba alikuwa hayumbi.

Mwengine alisema pua yake inatoka damu, huku mwengine akiomba ”ondoka katika shingo yake”.

Mtu huyo anaonekana ametulia kabla ya kuingizwa katika ambulansi na kuondoka naye.

Maafisa wa polisi wanasema kwamba hakuna silaha iliotumika wakati wa kisa hicho , na kwamba picha zimepelekwa katika shirika la ujasusi la kukabiliana na uhalifu la Minnesota, ambalo linachunguza kesi hiyo.

Siku ya Jumanne jioni maafisa walitumia vitoa machozi kutawanya maandamano ya umma nje ya kituo cha polisi mjini Mineapolis , kulingana na vyombo vya habari vya eneo hilo.

Mwandishi mmoja wa gazeti la The Star Tribune alituma ujumbe wa twitter kwamba alikuwa amepigwa na risasi bandia iliofyatuliwa na polisi.

Ripota mmoja wa runinga ya KTSV alituma ujumbe wa Twitter akisema kwamba waandamanaji walivunja vioo katika kituo hicho na kuchora maandishi machafu katika gari moja la polisi.

Maafisa wa polisi walisema katika taarifa yao awali kuhusu kifo cha Geore Floyd: Baada ya kupata habari zaidi, imebainika kwamba shirika la ujasusi nchini Marekani FBI litashirika katika uchunguzi huo.

Akizungumza kwa vyombo vya habari vya Marekani siku ya Jumanne, Afisa mkuu Arradondo alisema kwamba sera za kikosi cha polisi kuhusu kumdhibiti mshukiwa zitachunguzwa kama mojawapo ya uchunguzi huo.

Kulingana na chombo cha habari cha AP, maafisa wa polisi wa Minneapolis wanaruhusiwa kupitia sera ya kutumia nguvu kuweka magoti yao katika shingo ya mshukiwa iwapo kitendo hicho hakitaathiri njia za kupumua za mshukiwa.

Alipoulizwa kuhusu uchunguzi huo wa FBI Arradondo alisema , aliamua kuchukua uamuzi huo baada ya kupokea habari zaidi kutoka chanzo kimoja cha kijamii.

The post Marekani: Polisi wanne wafutwa kazi kufuatia kifo cha mtu mweusi appeared first on Bongo5.com.