Marekani imewawekea marufuku ya usafiri raia wa kigeni ambao wamekuwa Brazil katika kipindi cha siku 14 zilizopita. Taifa hilo la Amerika Kusini hivi karibuni limekuwa ngome la pili kuu la maambukizi ya virusi vya corona duniani.

Brazil imethibitisha kuwa zaidi ya watu 360,000 wameambukizwa corona, huku zaidi ya watu 22,000 wakifariki kutokana na baada ya wizara ya Afya ya nchi hiyo kutangaza Jumapili hali ilivyo.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani amesema kuwa udhibiti huo wa usafiri utasaidia kuhakikisha hakuna maambukizo mapya yataletwa nchini.

“Hatua ya leo itasaidia kuhakikisha raia wa kigeni ambao wamekuwa Brazil hawatakuwa chanzo cha maambukizi mapya ya corona nchini mwetu,” Ilisema taarifa ya Msemaji wa Ikulu ya Marekani Kayleigh McEnany.

Hofu ya maambukizi

Watu wasiokuwa raia wa Marekani na ambao walikuwa Brazil ndani ya muda wa wiki mbili kabla ya kuomba idhini ya kuingia Marekani watazuiliwa kuingia nchini humo. Hatua hiyo haitaathiri biashara kati ya nchi hizo mbili.

Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa Mei 28 (03:59 GMT).

Marufuku hiyo ya usafiri haitawajumuisha raia wa Marekani, wanadoa, wazazi, walezi halali, au mto wa raia wa Marekani ama wakaazi wa kudumu, na ndugu walio na umri wa chi ya miaka 21.

“Uwezo wa watu walioambukizwa kupitisha virusi upo juu hasa kutoka kwa wale wanaotaka kuingia Marekani kutoka [Brazil] hali ambayo huenda ikatishia usalama wa mfumo wetu wa usafirishaji na miundombinu na usalama wa kitaifa,” ilisema katika amri hiyo ilichapishwa na Ikulu ya Marekani siku ya Jumapili.

Awali mashauri wa kitaifa wa Ikulu ya Marekani Robert O’Brien aliiambia CBS “Kabili taifa” akiashiria kuwa marufuku ya usafiri tdhidi ya Brazil ilitarajiwa wakati wowote.

“Tunatumai kuwa marufuku hiyo itakuwa ya muda, kutokana na hali ilivyo nchini Brazil, tutachukua kila hatua kulinda watu wa Marekani,” Bw. O’Brien alisema.

Aliongeza kusema “Tunatathmini hali ilivyo katika mataifa mengine kwa kuangazia kila moja kivyake”.

Rais wa Marekani Donald Trump mapema wiki hii aligusia kuwa anatafakari kuwawekea marufuku wasafiri kutoka Brazil.

Marekani kwa sasa inaongoza duniani kwa kuwa na visa vingi vya maambukizi ya virusi vya corona. Ina zaidi ya watu milioni 1.6 waliothibitishwa kuwa na virusi na vifo karibu 100,000 vinavyohusishwa na virusi hivyo.

Tangazo hilo la Jumapili ni hatua ya hivi punde uliyochukuliwa na Marekani katika juhudi za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Raia wa kigeni ambao wamezuru nchi za China, Iran, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, Ungereza na Jamhuri ya Ireland tayari wamezuiliwa kuingia Marekani.

Canada na Marekani pia hivi karibuni zimekubaliana kurefusha muda wa kufunga mipaka yao ya pamoja kwa usafiri ambao sio wa muhimu.

Hali ikoje?

Brazil hivi karibuni iliipiku Urusi katika maambukizi ya virusi. Rais Jair Bolsonaro amepuuza mara kadhaa hatari inayotokana na virusi vya corona.

Idadi ya vifo nchini Brazilimeongezeka mara mbili zaidi katika kipinda cha karibu wiki mbili, ilikilinganishwa na kila miezi miwili nchini Uingereza, miezi minne Ufaransa na miezi mitano Italia.

Wataalamu wameonya kuwa idadi halisi ya walioambukizwa virusi huenda ikawa juu zaidi kutokana na ukosefu wa upimaji.

Ongezeko la vifo na maambukizi ya virusi vya corona nchini Brazil bila shaka inawatia hofu viongozi duniani, lakini rais Jair Bolsonaro hajaonesha dalili ya kuuchukulia ugonjwa huo kwa uzito unaostahili.

Kwa mara nyingine tena siku ya Jumapili, alionekana akitangamana na mamia ya wafuasi wake mjini Brasilia – bila kuvalia barakoa.

Chanzo BBC

The post Marekani: Hakuna raia wa kigeni kutoka Brazil atakayeruhusiwa kuingia Marekani kisa Corona appeared first on Bongo5.com.