Maelfu ya watu walifanya maandamano jana nchini Ujerumani katika wimbi la maandamano linalozidi kuongezeka ambalo limemshtua hata kansela wa nchi hiyo Angela Merkel.
Waandamanaji hao walighadhabishwa na vikwazo vilivyowekwa, madai ya mipango ya chanjo ama ya uangalizi wa serikali. Awali maandamano hayo yalianza na waandamanaji wachache lakini idadi hiyo imekuwa ikiongezeka katika wiki za hivi karibuni kufikia maelfu ya watu katika miji mikuu ya Ujerumani.
Zaidi ya waandamanaji elfu 5 walikusanyika mjini Stuttgart, takriban 1500 mjini Frankfurt na takriban elfu 1 mjini Munich. Moja ya bango mjini Stuttgart liliandikwa kuwa ”corona ni bandia” huku lingine likiwa na ujumbe kwamba kujiweka mbali na watu, barakoa, kufuatilia, chanjo havifai.
Maandamano hayo yanayoongezeka yameibua ulinganishaji na maandamano dhidi ya waislamu (pegida) ya wakati wa mzozo wa wakimbizi barani Ulaya wa mwaka 2015 na kuibua maswali kuhusu iwapo ufuasi mkubwa wa Merkel kuhusu jinsi anavyolishughulikia janga la corona huenda ukafifia.
The post Maelfu ya watu waandamana Ujerumani, wachoshwa na vikwazo vya Corona ”Corona ni bandia” appeared first on Bongo5.com.