Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un hakufanyiwa operesheni wala kupatiwa matibabu yoyote ya kiafya licha ya kuendelea kuwepo uvumi juu ya afya yake hata baada ya kuonekana hadharani kwa mara ya kwanza katika kipindi cha wiki tatu.

Hayo ni kulingana na afisa mmoja mwandamizi katika ofisi ya Rais wa Korea Kusini ambaye amewaambia waandishi habari leo kuwa serikali mjini Seoul imejiridhisha kwamba Kim hakuwa na tatizo lolote la kiafya hivi karibuni.

Korea Kaskazini ilisema jana Kim alihudhuria hafla ya kukamilika ujenzi wa kiwanda cha mbolea mjini Pyongyang, na kuonekana hadharani kwa mara ya kwanza.

Licha ya picha za video kumuonesha Kim akitabasamu na kukata utepe, vyombo vya habari na wafuatiliaji wa hali ya mambo bado wanashuku hali ya afya ya kiongozi huyo wakisema alionekana akitembea kwa tabu kwenye eneo la kiwanda.

The post Korea Kusini: Kim Jong Un hakufanyiwa upasuaji  appeared first on Bongo5.com.