Serikali ya Korea Kusini imesema leo wanajeshi wake wamefyatuliana risasi na wanajeshi wa Korea Kaskazini katika eneo lisilo na shughuli za kijeshi linalozitenganisha Korea mbili. 

Taarifa ya mkuu wa majeshi wa Korea Kusini imesema kituo kimoja cha walinzi kilishambuliwa kwa risasi kadhaa kutoka upande wa kaskazini, lakini hakuna aliyejeruhiwa.

 Afisa huyo wa jeshi amesema jeshi la Korea Kusini lilifyatua risasi kujibu shambulizi hilo na kutoa onyo kwa wanajeshi wa upande wa kaskazini. 

Makabiliano hayo ya nadra yametokea siku moja tangu vyombo vya habari vya Korea Kaskazini kuripoti kuwa kiongozi wake Kim Jong Un ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza katika kipindi cha karibu wiki tatu. 

Kutoonekana kwa Kim kulizusha uvumi kuhusu hali yake ya afya na wasiwasi juu ya hatma ya taifa hilo