Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM), Humphrey Polepole zinatakiwa kupuuzwa.

Amesema wao kama chama hawajawahi kusema chochote kuhusiana na ugonjwa wa Corona.

“Walijifungia kusikojulikana na wamejitokeza leo kutuaminisha kwamba ugonjwa umeisha wakati hatupimwi na maabara ya taifa imefungwa na inachunguzwa. Puuzeni aliyosema tujilinde,” andika Mrema katika ukurasa wake wa Twitter.


Polepole, amesema amewashangaa viongozi wa upinzani ambao walikuwa wakikosoa namna mbalimbali ambazo Rais Dk John Pombe Magufuli alizokuwa akizichukua kushughulikia tatizo la ugonjwa wa Covid-19.

Polepole ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM Lumumba jijini Dar kwa ajili ya kutoa shukrani mbalimbali kwa Watanzania na wahudumu ambao walikuwa mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Polepole amesema, viongozi hao wa upinzani hususan Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe walikuwa wakiitaka Serikali ifungie baadhi ya mikoa ambayo ina maambukizi makubwa bila kujua kufanya hivyo kungekwenda kuwaathiri Watanzania wengi zaidi wa kipato cha chini.

“Wako watu hapa Tanzania hasa kutoka vyama vya upinzani, walikwenda mbele wakasema, baadhi yao si wote. Wakasema tuufunge mkoa wa Dar es Salaam, tufunge Arusha…halafu tukifunga tutakula wapi? Hivi kweli Serikali ingeweza kutulipa mishahara?” alisema Polepole.

Alisema badala yake, Rais alielekeza zaidi watu kujilinda kwa kuchukua hatua zinazoelekezwa na wataalam wa afya pamoja na kutumia tiba mbadala.

“Rais wetu akasema msisahau mbona tuna mbinu nyingi tu hapa za asili wala si uganga? Kuna kujifukiza kula tangawizi, kula vyakula ambavyo vinaongeza kinga ya mwili, watu walipokea kwa muitikio mkubwa sana.