DAR: Mbivu na mbichi juu ya kesi ya uharibifu wa mali inayomkabili staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Mondi’ pale Mtaa wa Mpakani B, Kijitonyama jijini Dar, itajulikana Julai 3, mwaka huu.

Uharibifu huo unadaiwa kufanyika mahali hapo zilipokuwa Studio za Wasafi Classic Baby (WCB) kabla ya kuhamia Mbezi- Beach jijini Dar.

Kesi hiyo iliahirishwa kwa mara nyingine Mei 7, mwaka huu katika Mahakama ya Ardhi Kinondoni iliyopo Mwananyamala, Dar na Hakimu Laurent Wambili.

Sasa, kesi hiyo inayofuatiliwa kwa ukaribu na gazeti hili imepangwa kusikilizwa Julai 3 baada ya pande zote kutoa udhuru; yaani upande wa Mondi unaowakilishwa na Wakili Frank Modestus na mlalamikaji Maulid Wandwi.

Awali, Mondi alitakiwa kulipa kodi ya pango aliyokuwa akidaiwa ambayo ni ya mwaka na miezi minne ambapo mlalamikaji (mwenye nyumba) Wandwi aliomba kulipwa kodi ya mwaka na kusamehe miezi minne iliyobaki, lakini wakili wa upande wa Mondi alikuja na maelezo kuwa, mteja wake amesema atafanya matengenezo ya nyumba na kulipa miezi minne tu, badala ya kodi ya mwaka mzima.

Kufuatia kukosekana kwa muafaka kati ya mdaiwa Mondi na mlalamikaji Wandwi, kesi itasikilizwa tena Julai 3 ili kufikia makubaliano baina ya pande zote.

Mondi anakabiliwa na kesi hiyo ya uharibifu wa vitu vyenye thamani ya shilingi milioni 33.7 kwa mujibu wa wasanifu majengo waliofanya uchunguzi wa vitu vilivyoharibika ndani ya nyumba aliyokuwa amepanga na kuitumia kama studio ambayo ni mali ya Wandwi.

Stori: HAPPYNESS MASUNGA, Ijumaa