Katika hatua ya kukabiliana na mbu waenezao ugonjwa wa Malaria nchini, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii jinsia, Wazee na Watoto kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeendelea kutekeleza kampeni mbalimbali za kudhibiti Malaria ikiwa ni miongoni mwa hatua za kutokomeza ugonjwa huo hadi kufikia mwaka 2030.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Peter Gitanya amesema kuwa Kampeni hiyo ambayo imelenga kugawa vyandarua 719,254 kwa mkoa wa Rukwa ni muendelezo wa kampeni kubwa tatu za uhamasishaji wa ugawaji wa vyandarua kwa kaya zilizowahi kufanyika miaka ya 2009, 2010 na 2015/2016 na kuongeza kuwa Bohari ya Dawa (MSD) itahusika na usafirishaji wa vyandarua kutoka maghala yao katika kila mkoa hadi kituo cha ugawaji katika Kijiji ama mtaa husika.

“Halmashauri ambako kampeni itafanyika ni zile halmashauri ambazo zina kiwango cha chini cha umiliki wa vyandarua, chini ya 40%, na pia maambukizi ya malaria yapo katika kiwango cha juu na cha kati, Halmashauri zenye kiwango cha chini cha uwepo wa malaria zilizozungukwa na halmashauri zenye kiwango cha juu na cha kati cha uwepo wa malaria na halmashauri ambazo mpango wa ugawaji wa vyandarua kupitia wanafunzi shuleni haufanyiki,” Alisisitiza.

Katika kusisitiza hilo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wahusika wote wa kampeni hiyo kushirikiana kwa karibu katika kufikisha elimu iliyosahihi kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya vyandarua na kuongeza kuwa ili kufanikisha mpango wa serikali kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha tunapambana na maradhi hayo ili kuwa na jamii yenye afya na yenye uwezo wa kuzalisha.

“Mimi nitoe wito tu kwamba ili mpango huu uweze kufanikiwa, tunahitaji tushikamane, tushirikiane kwa nguvu zote, kufikisha elimu iliyosahihi kwa wananchi, vinginevyo tusipotoa elimu kwa nguvu zote na watu wakaelewa tunaweza tukatwanga maji kwenye kinu, kwahiyo jambo kubwa liwe ni elimu, elimu iwafikie wananchi kwa nguvu zote, kama tulivyoanza hapa kushirikishana hivi, tuendelee kushusha kuwashirikisha wadau mbalimbali,” Alisema.

Aidha, aliishauri wizara ya afya na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kuona namna ya kufanya utafiti juu ya miti shamba inayotumika kufukuza mbu katika baadhi ya maeneo vijijini ili wananchi waweze pia kutumia miti hiyo kwa kuipanda maeneo ya nyumba zao na hatimae kuwafukuza mbu hao.

Kampeni hiyo itagawa vyandarua 7,097,565 katika Halmashauri 50 kutoka katika mikoa 10 nchini ikiwa na lengo la kugawa vyandarua hivyo vyenye dawa kwa walengwa kwa asilimia 100 na Kwa mkoa wa Rukwa kampeni hiyo itagawa vyandaru katika halmashauri zote nne za mkoa kwa kuwatambua walengwa na kuwahamasisha juu ya matumizi na utunzaji wa vyandarua hivyo.