SALVATORY NTANDU
Katika jitihada za kuunga mkono Serikali katika mapambano dhindi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu  inayosababishwa na virusi vya Corona Mamlaka ya Maji Kahama na Shinyanga (KASHUWASA) imekabidhi vifaa vya kunawia mikono  kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Anamringi Macha ili viweze kusaidia katika mapambano ya dhidi ya COVID 19.

Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi  vifaa hivyo iliyofanyika Mei 7 mwaka huu katika Mjini Kahama Mkurugenzi wa KASHUWASA, Joshua Mageyekwa amesema vifaa hivyo vitatumika  kuwasaidia wananachi hasa kwenye sehemu yenye mikusanyiko mikubwa kama vile kwenye masoko minada na hospitali.

“Bodi ya wakurugezi ya KASHUWASA ilikubaliana kugawa vifaa vya kunawia mikono katika maeneo yote ambayo sisi tunatoa huduma ambapo leo katika wilaya ya kahama tunatoa mapipa 15 yenye ujazo wa lita 210 ili kuisaidia jamii katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID 19,”alisema Mageyekwa.

Aliongeza kuwa KASHUWASA itaendelea kushirikiana na serikali katika janga hili ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki ambazo zitawawezesha kuchukua tahadhari sambamba na kuwakinga wengine kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.

Awali akipokea vifa hivyo mkuu wa wilaya hiyo Anamringi Macha amesema msaada huo umekuja katika muda muafaka na atahakikisha  mapipa hayo yanawekwa katika maeneo yote ya umma yenye mikusanyiko mikubwa ya watu katika halmashauri tatu za Ushetu,Mji na Msalala.

“Nitoe shukurani zangu kwenu KASHUWASA kwa msaada wenu kwa wananchi wa wilaya ya kahama,awali tulianza kutumia ndoo ndogo kwaajili ya kunawia mikono lakini hivi sasa nyinyi mmetupatia mapipa makubwa tutahakikisha yanatumika katika maeneo yote ya umma,”alisema Macha.

Macha amewaomba wafanyabiashara na watoa huduma wengine katika maeneo yao kuhakikisha wanalinda afya za wateja wao kwa kuhakikisha wanachukua tahadhari kwa kunawa mikono kwa maji safi na salama ili kujikinga na Janga la ugonjwa wa COVID 19.

“Kama hakuna wateja hakuna biashara ni wajibu wenu wafanyabiashara kuhakikisha mnaweka mazingira rafiki ili kuendeleza biashara zenu,wamiliki wa baa na watoa huduma za usafiri himizeni wateja wenu wanawe mikono kabla ya kupata huduma au kuingia kwenye basi,”alisema Macha.

Sambamba na hilo Macha alisema kuwa mwitikio wa wananchi katika unawaji wa mikono katika maeneo mbalimbali umekuwa mkubwa ikilinganishwa na hapo awali ambapo hivi sasa elimu juu ya kujikinga na ugonjwa huu imeanza kueleweka kwani katika maeneo mengi huwezi kupata huduma bila kunawa mikono au kuvaa barakoa.

Mwisho.