SALVATORY NTANDU
Baada ya kuwepo kwa Malalamiko ya Wakulima wa tumbaku kutolipwa fedha na kampuni za ununuzi wa zao hilo katika msimu wa 2019/20 katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Baraza la Madiwani  la  Halmashauri hiyo limeagiza kufanyika kwa uhakiki wa madai hayo kabla kufanyika kwa Masoko  mapya ya mwaka 2020/21.

Uamuzi huo ulitolewa Aprili 30 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya hiyo, Juma Kimisha katika kikao cha kawaida cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2019/20 kuanzia Januari hadi Marchi baada ya kupokea taarifa mbalimbali za maendeleo zilizotekelezwa na serikali.

Alisema kuwa katika vyama vya Msingi Kangeme,Tumaini na Ilomelo wakulima wake wanazidai kampuni za ununuzi wa zao hilo zaidi ya Milioni 80 baada ya kuchukua mazao yao katika Msimu uliopita na hadi sasa hawajui ni lini watapata stahiki zao.

“Diwani wa Kata ya Ulowa Paschal Mayengo aliwasilisha malalamiko ya wakulima wake hapa ya kutolipwa fedha na  kampuni za Jaspay na Magepa ambazo zinafikia Dola elfu 35000 ambazo mpaka hivi sasa hawajalipwa huku msimu mpya ukitarajiwa kufunguliwa Mwezi Mei mwaka huu,”alisema Kimisha.

Nae Diwani wa kata ya Igunda Tabu Katoto alishauri ofisi ya Mkurugenzi kufuatilia kwa kina Madai yao ili kudhibiti vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na baadhi ya kampuni hizo ambazo hazina nia ya kuwakomboa wakulima wa Ushetu.

“Tuweke msisitizo kwa kampuni zote za ununuzi wa zao hili zihakikishe zinajenga  ofisi ili wakulima wetu wasiwe wanahangaika na itasaidia kwabana viongozi wake ikilinganishwa na hivi sasa ambako hatujui wamiliki wake na ni wapi wapatikana,”alisema Katoto.

Akipokea Maelekezo ya kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Michael Matomora alikiri kuwepo kwa madai ya wakulima hao na kuomba kupewa muda kwaajili ya kufanya uhakiki ili kujua uhalali wake.

“Nipeni muda ili niwezekufanya kazi hii kwa ukamilifu niwaahidi nitatoa taarifa kwa kina katika kikao cha Kamati ya fedha ambacho kitaketi hivi karibuni,”alisema Matomora.

Mwisho.