Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Kigoma imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Kajana, Wilaya ya Buhigwe, Doto Simoni (21), kifungo cha miaka 15 jela baada ya kukiri kumuua bila kukusudia ndugu yake Manase Ezekieli kwa kumpiga na mti usoni na kufariki dunia papo hapo.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji wa Mahakama hiyo, Athumani Matuma baada ya mshitakiwa huyo kukiri kosa.

Matuma alisema mahakama hiyo inatoa adhabu kali kwa mshitakiwa huyo ili iwe fundisho kwake na kwa vijana wengine wenye tabia za kikatili kama yake.

Alisema mshitakiwa alimuita Manase ambaye kwa sasa ni marehemu aliyekuwa akiishi Wilaya ya Kasulu amfuate kwa ajili ya kumpa dawa ili asilogwe na wachawi.

Jaji Matuma alisema alipofika, mshitakiwa alimchukua ndugu yake huyo na kumpeleka kando ya mto Chai na kumwambia akae chini na kufumba macho na kisha anyanyue uso juu, ndipo alipochukua mti na kumpiga usoni kitendo kilichomfanya aanguke chini na kufariki dunia papo hapo.

Vile vile, alisema mshitakiwa alirudi nyumbani kwake na kunyamaza kimya na kudai kuwa hajui ndugu yake alipo.

Alisema ndugu wengine wa marehemu walienda kutoa taarifa polisi za kupotea kwa ndugu yao na walianza kumtafuta sehemu mbali mbali.

Alisema ndugu wengine wa marehemu pamoja na polisi walimshuku mshitakiwa na kumkamata na kumbana ndipo alipokiri kumuua.

Jaji Matuma alisema baada ya kufika eneo la tukio, walikuta mifupa ya binadamu na nguo za marehemu ambazo ni shati, suruali, bukta na mti, ambazo ndugu wa marehemu walizitambua kuwa ni za marehemu Ezekiel.

Jaji Matuma alisema kitendo alichokifanya mshitakiwa huyu ni cha kikatili pamoja na kukiri kosa lake mahakama inamtia hatiani kwa kosa la kuua ndugu yake bila kukusudia.

Alisema upande wa mashitaka ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Benedict Kivuma.

Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili wa kujitegemea Diana Damson, uliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa bado mdogo na amekaa mahabusu kwa miaka miwili.

Hata hivyo, Jaji Matuma alitupilia mbali utetezi huo.