Maafisa wa polisi nchini Iran wamemkamata mwanamume mmoja anayetuhumiwa kumuua mwanawe wa kike mwenye umri wa miaka 14 katika kile kinachotajwa kuwa ‘mauaji ya heshima’ ambayo yamezua hisia kali na ghadhabu.
Romina Ashraf alitoroka nyumbani kwao katika mkoa wa Gilan na mpenzi wake mwenye umri wa miaka 35 baada ya babake kupinga waowane, vilisema vyombo vya habari vya eneo hilo.
Wawili hao walikamatwa na maafisa wa polisi kabla ya Romina kurudishwa nyumbani licha ya kuwaambia maafisa hao kwamba alikuwa anahofia maisha yake.
Alhamisi iliopita , anadaiwa kushambuliwa na babake katika chumba chake.
Chombo cha habari cha Gilkhabar.ir kiliripoti kwamba Romina alikatwakatwa na baadaye babake akatoka nje na kifaa alichokitumia kufanya kitendo hicho na kukiri kumuua.
Siku ya Jumatano, baadhi ya magazeti yaliangazia tukio hilo katika ukurasa wao wa kwanza.
“Nyumba ya baba isio salama”, kilisema kichwa cha habari cha gazeti linalounga mkono mabadiliko Ebtekar, ambalo lilizungumzia kuhusu ukosefu wa sheria zilizopo kuwalinda wanawake na wasichana.
Wakati huohuo, Hashtag ya #Romina_Ashrafi imetumika zaidi ya mara 50,000 katika mtandao wa Twitter, huku watumizi wake wengi wakilaani mauaji hayo na kuhoji sheria zinazowalinda wanawake kwa jumla.
Shahindokht Molaverdi, makamu wa rais wa zamani wa shirika la wanawake na masuala ya familia na katibu wa sasa wa shirika la kijamii linalolinda haki za wanawake aliandika: Romina sio wa kwanza na wala hatakuwa wa mwisho wa ‘mauaji ya heshima’.
Aliongezea kwamba mauaji kama hayo yataendelea hadi pale sheria na tamaduni katika jamii hazitakuwa tishio.
Sheria za kiislamu nchini Iran huwapunguzia adhabu kina baba na ndugu wa familia ambao wamepatikana na hatia ya mauaji ama hata kuwapiga wanao katika unyanyasaji wa kinyumbani au ‘mauaji ya heshima’.
Lakini je ‘mauaji ya heshima’ ni ya aina gani?
Ni mauaji ya ndugu wa familia ambaye anadaiwa kuleta aibu miongoni mwa watu wa familia.
Wanaharakati wanasema kwamba sababu za kufanyika kwa mauaji hayo ni kwamba mwathiriwa:
- Alikataa kuolewa
- Alikuwa mwathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia au ubakaji
- Alishiriki ngono nje ya ndoa hata iwapo ni madai tu.
Iwapo mwanamume atapatikana na hatia ya kumuua mwanao nchini Iran , adhabu yake ni kati ya miaka mitatu hadi kumi ,badala ya hukumu ya kifo ama ulipaji wa diyeh{fedha za damu} kwa visa vya mauaji.
Hakuna takwimu kuhusu visa vya mauaji ya heshima nchini Iran, lakini wanaharakati wa haki za kibinadamu waliripoti mwaka uliopita kwamba vinaendelea kuwepo hususana miongoni mwa wakaazi wanaoishi katika maeneo ya mshambani kulingana na wizara ya masuala kigeni nchini Marekani.
The post IRANI: Baba amuua binti yake kisa kafunga ndoa kwa siri, Adai ni mauaji ya heshima appeared first on Bongo5.com.