Wahispania waliingia mitaani siku ya Jumamosi kufanya mazowezi ya kukimbia mitaani, kupanda baisikeli  na  michezo mingine  kwa mara ya kwanza  kufuatia  siku 48 za kulazimika  kubakia  majumbani mwao.

Wakati huo huo baadhi ya  mataifa ya Ulaya  kwa tahadhari yalilegeza vizuwizi vya kutoka nje, wakati Urusi na Ujerumani zimeripoti ongezeko la maambukizi.

Wakati serikali zikitafakari kuondoa vizuwizi vya  kuwataka  wananchi  kubakia  majumbani ili kuanzisha tena  uchumi wao, maafisa nchini Marekani  wameleta  matumaini kiasi  kwa  kuidhinisha  dawa ya  majaribio  ili  itumike  kwa wagonjwa  wa ugonjwa wa  COVID-19

Uamuzi  huo  ulikuwa  wa  hivi  karibuni  kabisa   katika  hatua  za dunia  kutafuta  dawa  na  chanjo  kwa ajili  ya  virusi  vya  corona, ambavyo  vimesababisha  nusu  ya  binadamu  dunia kuwamo  katika  vizuwizi vya  kutoka  nje na  kuuweka  uchumi  wa  dunia  kuelekea katika  mporomoka  mbaya  kabisa  tangu mdororo  mkuu  katika miaka  ya  1930.

Virusi  sasa  vimewauwa  zaidi  ya  watu 242,000 duniani  kote, kwa  mujibu wa  idadi  iliyowekwa  pamoja  na  shirika la  habari  la  AFP, na  walioambukizwa  wanafikia  milioni 3.4  tangu kuzuka  mara  ya  kwanza  virusi hivyo nchini  China mwishoni  mwa  mwaka jana.

Kukiwa na  ishara  kwamba  janga  hili  linapungua  kasi  katika mataifa  yale yaliyoathirika zaidi , mataifa  ya  Ulaya  pamoja  na baadhi  ya  sehemu  za  Marekani  yameanza  kuondoa  vizuwizi kujaribu kurejesha  hali  ya  maisha  kuwa  ya  kawaida  katika uchumi  ambao ulioathirika  kutokana  na  wiki  kadhaa  za kufungwa.

Watu watembea mitaani

Kuanzia  Madrid  hadi Mallorca, Wahispania  walimiminika  mitaani baada  ya  kuruhusiwa  kufanya  mazowezi na  kutembea  huru  nje baada  ya  serikali  kulegeza wiki  saba za  udhibiti  mkubwa  wa kuwataka  wananchi  wake  kubakia majumbani  katika  nchi  hiyo iliyokuwa  na  moja  ya  idadi  ya  juu  kabisa  ya  vifo  vilivyofikia zaidi  ya  25,000. “Baada  ya  wiki  kadhaa za  kufungiwa, nilikuwa nahitaji  sana  kutembea  nje, kukimbia, na  kuona  dunia,” alisema mshauri  wa   masuala  ya  fedha Marcos Abeytua  mjini  Madrid. “Jana  nilikuwa  kama  mtoto  katika  mkesha  wa  krismass.”

The post Hispania: Watu waruhusiwa kutembea nje kwa mara ya kwanza appeared first on Bongo5.com.