Viongozi wa dunia wameahidi kuchangisha Euro Bilioni 7.4 kwa ajili ya kufanya utafiti na kutengeneza chanjo dhidi ya virusi vya corona. Serikali, wafadhili na mashirika ya kimataifa yameahidi kuchangisha fedha hizo.

Symbolbild Corona-Virus Impfstoff (picture-alliance/dpa/Geisler-Fotopress)

Viongozi wa dunia wamesema chanjo yoyote itakayopatikana itapaswa itolewe kwa wote na kwa bei ambayo wote wataweza kuimudu. Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema juhudi zaidi zitahitajika katika miezi ijayo. Ameongeza kusema kwamba mkutano huo ni mwanzo tu wa juhudi ndefu.

Umoja wa Ulaya umeahidi kuchangia Euro bilioni moja. Ujerumani imesema itatoa Euro milioni 525 na Ufaransa itatenga Euro milioni 500. Nchi nyingine zilizoahidi kuchangia ni pamoja na Norway ambayo si mwanachama wa Umoja wa Ulaya bali ni mwenyekiti mwenza wa juhudi hizo.

Uhispania ambayo ni miongoni mwa nchi za barani Ulaya zilizokumbwa vibaya na mambukizi ya virusi vya corona pia imechangia. Mpaka sasa watu zaid ya 25,000 wameshakufa kutokana na virusi hiyvo nchini humo.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema fedha zitakazotolewa na Umoja huo kwa ajili ya chanjo itakayotengenezwa ni juhudi za pamoja za nchi wanachama wa jumuiya hiyo. Wenyeviti wenza wa mkutano huo ni Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia, Japan na Saudi Arabia ambayo kwa sasa ni mwenyekiti wa kundi la nchi za G20.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen (DW)Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen

Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel amesisitiza kwamba juhudi zinazofanywa zinapaswa kulingana na uzito wa janga lililopo.

Viongozi wa Marakeni na Urusi hawakushiriki kwenye mkutano huo, na China ambako mlipuko wa maambukizi ya corona ulizuka, iliwakilishwa na balozi wake kwenye Umoja wa Ulaya. Waziri mkuu wa Norway Erna Solberg amesikitika kwamba Marekani imeamua kujiweka kando.

Kabla ya mkutano huo viongozi kadhaa wa Ulaya walitia saini barua bayana iliyochapishwa magazetini, ya kuliunga mkono shirika la afya duniani WHO na mashirika ya kimataifa yanayoshiriki katika  juhudi za kutafuta chanjo.

Mataifa zaidi ya 30, Umoja wa Mataifa, mashirika ya misaada, wakfu wa Bill na Melinda Gates, na taasisi za utafiti ni sehemu ya juhudi za kukusanya michango kwa ajili ya kupatikana kwa chanjo dhidi ya virusi vya corona. Mpaka sasa watu milioni 3 na nusu wameambukizwa virusi vya corona na zaidi ya laki mbili na elfu arobaini wamekufa duniani kote kutokana na COVID -19.

The post Euro Bilioni 7.4 kuchangishwa kutafuta chanjo ya Corona appeared first on Bongo5.com.