Rais wa Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, ameonesha kushangazwa na maamuzi ya Rais wa Awamu ya Tano Dkt John Pombe Magufuli, baada ya kumfukuza mfanyakazi Msukuma wa Ikulu, ambaye alishindwa kununua incubator ya kutotoa mayai ya Tausi.


Dkt Kikwete ameyabainisha hayo leo Mei 30, 2020, jijini Dodoma, wakati wa zoezi la kukabidhiwa ndege aina ya Tausi kwa Marais wastaafu pamoja na mjane wa Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere.

"Mimi ndiyo mdogo nasema kwa niaba ya Wazee hawa, tunatoa shukrani kwa moyo wako wa upendo kwa kutupatia hawa ndege, tulikuwa tunawatamani lakini ukitoka nao, ukafika nao Msoga, watu watasema amepora, pia nakupongeza kwa maamuzi ya incubator lakini yule Msukuma sikukuambia umfukuze, lakini nilieleza tu masikitiko yangu" amesema Dkt Kikwete.

Aidha awali wakati akizungumza, Rais Magufuli amewapongeza Marais wote Wastaafu walioshiriki kuwatunza Tausi hao.