Jeshi la Polisi mkoani Geita linawashikiliwa watu sita kutoka kwenye familia mbili ya muoaji na muolewaji kwaajili ya uchunguzi zaidi kufuatia kifo cha Samweli Juma mwenye umri wa miaka 25, mkazi wa Kijiji cha Nyarutefi, katika hifadhi ya Pori la Biharamulo wilayani Chato ambaye amefariki kwa kupigwa na kitu kizito kichwani baada ya mvutano wa familia hizo mbili waliokuwa wakigombea mbuzi wawili waliotolewa kama Mahari.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita, Mponjoli Mwabulambo anaelezea chanzo cha kijana huyo kupoteza maisha.

”Wakati wanajadiliana na kufikia makubaliano, ndipo ulipotokea mzozo, mahari zilizokuwa zimetolewa pale zilikuwa ni Mbuzi wawili.”

Kamanda Mwabulambo ameongeza ”Lakini katika mazingira ambayo upande huu wa waoaji, haukupenda mbuzi mmoja atolewe, wakidai kwamba mbuzi huyo alikuwa ni kwaajili ya shughuli zao za matambiko.”

”Kwa hiyo mzozo uliendelea, na kadiri walivyokuwa wanapambana, upande mmoja unamrudisha mbuzi upande mwingine unamng’ang’ania mbuzi, kwa maana kwamba waondoke naye.”

”Ilifikia mahala sasa wakashindwa kuvumiliana wao kwa wao, kwa hiyo huu upande wa waoaji, wakamrushia bwana mmoja Kazimili Enosi ambaye ndiye Baba wa yule binti anayeolewa katika nyumba hiyo, alirushiwa na kitu kizito ambacho baadaye akapata majeraha kichwani. Hali ambayo ilipelekea sasa naye arudishe.”

”Kwa hiyo akarushia kitu kizito upande ule mwingine wa pili, ambapo moja kwa moja ulikuja kumpata mtu mmoja ambaye alijulikana kwa jina la Samweli Juma, Msukuma mwenye umri wa miaka 25. Huyu kwa sasa tunavyoongea ni marehemu.”

Mpaka sasa Jeshi la Polisi linawashikilia watu sita kutoka kwenye familia mbili ya muoaji na muolewaji kwaajili ya uchunguzi zaidi.

”Watuhumiwa wote hao tunawashikilia na tunaendelea na upelelezi wa tukio hili ili kuweza kujua na kujiridhisha mazingira haya yaliopelekea kifo cha Bwana Samweli Juma ambaye ndiyo kaka wa muoaji.”

The post Baba mkwe asababisha kifo cha kaka wa Bwana harusi kwa kugombea Mbuzi wa Mahari appeared first on Bongo5.com.