Mfugaji Lenina Saturo, amesimulia huku akitokwa na machozi namna ambavyo alilazimika kuwaweka watoto wake wa kike rehani ili aendeshe kesi ya kugomboa ng’ombe wake 311.
Saturo alisimulia kuwa baada ya mifugo yake kukamatwa kwa madai kuwa imeingia hifadhi ya …kesi ilipelekwa mahakamani.
Alisema baada ya hukumu kutoka Oktoba 3, mwaka 2018 hadi sasa hajapata mifugo yake na kujikuta akibaki peke yake baada ya wake zake kurudi kwao na watoto wakiwa rehani.
Saturo alisimulia kuwa akiwa hospitalini akiuguza majeraha baada ya ajali aliyoipata, huku nyuma ng’ombe zake 311 zilikamatwa.
“Wadogo zangu na watoto waliokuwa nyumbani siku hiyo ndiyo waliosaidia, kwa sababu nilikuwa hospitali, baada ya ng’ombe kukosekana siku moja ndipo wakasema zimeibiwa na baadaye zilikutwa katika Wilaya ya Kondoa na kusema zimekamatwa kwenye hifadhi,” alisema.
Alisema vijana waliokuwa wakifuatilia mifugo hiyo nao walikamatwa kwa madai kuwa walichunga kwenye hifadhi.
“Baada ya kufuatiliwa Kondoa ikabainika hazikuingia kwenye hifadhi au kama ziliingia kule ni mbali, Mahakama ya Wilaya ya Kondoa iliamuru ziachiliwe na vijana waachiwe.
“Meneja alikata rufani kuja Dodoma na hukumu ilitoka Oktoba 3, mwaka 2018 mpaka leo sijapata mifugo yangu, nilipofuatilia mahakamani, waliitwa Mwendesha Mashtaka atoe vielelezi vya kuachia ng’ombe na hakuja.
Alisema waliitwa na Mbunge wa Kiteto, ambaye aliwataka wakachukue ng’ombe wao.
“Tukaambiwa kwamba ng’ombe wamekwenda kuhesabiwa na kati ya ng’ombe 311 walibaki 197, nina wake sita na watoto 43,” alisema.
Saturo alisema alijaribu kufuatilia kesi hiyo, lakini imeshindikiana kwa sababu hana nguvu hajabaki na chochote.
Ali sema watoto amewapeleka kwa ndugu zake na wake zake wametoroka kwenda kwao na mifugo yake hajaipata hadi sasa.
“Nikashindwa sina nguvu tena kwa sababu fedha niliyokuwa ninaendeshea kesi ilikuwa na riba nikawa nauza watoto,” alisema.
Saturo akisimulia huku akitokwa na machozi, alisema alikuwa akiuza watoto wake wadogo ili alipe riba na hajafanikiwa kupata ng’ombe.
“Ninapenda kuonana na Rais (John Magufuli), kwa sababu ninajua ni mtetezi wa wanyonge ninajua anajua walemavu na watoto yatima anawajua, ninamuomba kwa sababu huku hakuna haki.
“Niliposhinda kesi nilijua ni chombo cha haki, ninapenda kumuona Rais kama sijamuona ni bora ninywe sumu kwa sababu sina nguvu tena, ninajua Rais ni baba yetu tunamtegemea anajua wafugaji na watu wenye walemavu na wanyonge. Kama atanisaidia ili nipate hata kidogo ili nikawakusanye watoto wangu.”
Wakati Saturo akieleza hayo, Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), kimeeleza ukiukwaji wa sheria na uonevu unaofanywa na mamlaka za hifadhi dhidi ya mifugo ambapo hadi sasa iliyotaifishwa ni 1,955 na iliyouawa ni zaidi 5,000.
Kupitia tamko lao walilolitoa jana kwa pamoja na kusainiwa na Mwenyekiti wa CCWT, George Bajuta na Katibu Mkuu wake, Magembe Makoye, wafugaji wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hizo.
“Kumekuwa na utaifishaji wa mifugo usiozingatia sheria katika hifadhi mbalimbali za misitu na za wanyamapori ambao umesababisha umaskini na mateso kwa wafugaji,” walisema.
Viongozi hao walisema kuwa utaifishaji huo umefanyika maeneo mbalimbali nchini licha ya baadhi ya kesi zikiwa mahakamani na nyingine wafugaji wakiwa wameshinda.
SOURCE NIPASHE
The post Aweka watoto rehani kukomboa ng’ombe wake, aomba kuonana na Rais ”Kama sijamuona rais ni bora ninywe sumu” appeared first on Bongo5.com.