Mfanyabiashara wa madini na mbao, Jonas Mahenge (52) aliyekuwa akiishi Kata ya Uyole Jijini Mbeya, amejiua kwa kujipiga risasi mdomoni na kutokea utosini kwa kutumia bunduki yake baada ya kushindwa kurejesha mkopo wa Tsh milioni 100 aliouomba benki.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema tukio hilo limetokea Mei 18, 2020 saa tisa usiku, ambapo mfanyabiashara huyo alijipiga risasi kwa kutumia bunduki aina ya Pisto Browning yenye namba za usajili 00099307.

Kufuatia tukio hilo, Kamanda Matei amewashauri wananchi kuwa na mpango mkakati wakati wa kufanya shughuli za kiuchumi zozote kabla ya kuchukua mkopo wowote na kwamba kabla ya kufanya biashara yoyote wawashirikishe wataalamu wa biashara kwa ushauri ili washauri mapato na matumizi ya biashara zetu.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi limemtia nguvuni, Marko Kandonga (78) Mkazi wa Kilambo, Kata ya Njisi wilayani Kyela kwa tuhuma za kupatikana na nyara za Serikali bila kibali ikiwamo ngozi moja ya mnyama aina ya Komba, ngozi ya nyoka aina ya chatu na mkia wa Ngiri ambazo zote thamani yake bado haijapatikana lakini ufuatiliaji unaendelea.

The post Ajiua kwa kujipiga risasi ya mdomo kisa mkopo wa tsh milioni 100 appeared first on Bongo5.com.