IBRAHIM Ajibu, kiungo mshambuliaji wa Simba atakaa nyumbani kwa muda wa saa 48 bila kujumuika na wenzake wa Simba kutokana na adhabu aliyopewa na Kocha Mkuu Sven Vandenbroeck.
Vandernbroeck alimrudisha Ajibu nyumbani jana,Mei 29 na kusema kuwa anaweza kurejea Jumatatu ambayo ni Juni Mosi akikosekana kambini kwa muda wa siku mbili ambazo ni sawa na saa 48.
Sven amesema kuwa amelazimika kumrudisha nyumbani Ajibu kutokana na kosa lake la kuchelewa mazoezini.
"Adhabu ya Ajibu itamalizika Jumatatu ijayo hivyo ataweza kujumuika na wachezaji wenzake kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.Kosa la Ajibu ni kuchelewa mazoezini na sio jambo lingine.
“Ajibu alichelewa, nikiwa kocha nikawajibika kumrudisha nyumbani ikiwa ni sehemu ya kumuadhibu. Nadhani anaweza kurejea kikosini Jumatatu,” amesema kocha huyo.
Simba iliwasili kambini Mei 27 na kuanza maandalizi kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho.