Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewasilisha katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar muswada utakaoipa makali Sheria yake ya Vileo ya mwaka 1928 ambayo imeonekana kukiuka utamaduni na kusababisha uvunjifu wa amani.

Mswada huo uliowasilishwa juzi utafuta na kuandikwa upya sheria ya vileo na kuweka masharti ya kuzuia, kudhibiti na kusimamia uagizaji, kuhifadhi kwenye maghala, uuzaji, usambazaji na unywaji vileo na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Akizungumza kwa simu, Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii (Zati), Seif Miski alisema hivi karibuni kumekuwa na baa nyingi zilizofunguliwa katika maeneo ya vijijini zinazosababisha usumbufu.

“Wakati tukiunga mkono wa kufunga baadhi ya baa katika maeneo ya vijijini, tunadhani marekebisho hayo yanapaswa kubaki kwenye sehemu za starehe ili kuepuka uvunjifu wa haki za watu kwa kufanya ufuska na ugomvi karibu na maeneo ya watu,” alisema Miski.

Sheria hiyo itahusika kwa watu wanaoingiza, wanaohifadhi, wanaouza, wanaosambaza na kutumia pombe visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa muswada huo, hakuna mtu anayeruhusiwa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza au kuzalisha pombe Zanzibar.

Pia sheria hiyo ikipita, mtu au taasisi itakayokiuka sheria na kukukutwa na hatia, atahukumiwa kifungo cha miaka isiyopungua mitano au kulipa faini isiyopungua Sh5 milioni huku mitambo yake ya kuzalisha pombe ikitaifishwa na Serikali.

Muswada huo pia unazuia kutoa leseni ya kuuza au ruhusa ya maghala au uingizwaji wa vileo au kutolewa leseni Zanzibar kwa wazalishaji wa pombe au kwa mtu yeyote atakayekuwa na mkataba wa kuingiza au kuuza pombe.

Kama hiyo haitoshi, muswada huo unakataza mtu yeyote anayehusiana na wazalishaji au anayetaka kuwafadhili wazalishaji kwa lengo la kuingiza vileo visiwani humo.

Sheria hiyo ikipitishwa itawadhibiti watu kunywa au kukaribia maeneo ya aina yoyote ya vileo visiwani Zanzibar.

“Kwa maelezo hayo juu, mtu yeyote atakayekiuka kifungu cha sheria hii, akipatikana na hatia, atahukumiwa,” inasema sehemu ya muswada huo.

Pia, unakataza mtu yeyote, idara ya Serikali au taasisi yoyote kuuza au kutunza vileo vinavyochochea ulevi bila kuwa na leseni au kuweka ghala la vileo.

Kwa hali hiyo, mtu atakuwa na hatia ya kukutwa na kileo, isipokuwa mtu aliye na leseni chini ya sheria hiyo au mtu aliyenunua na kumiliki kileo hicho iwe ni kwa matumizi binafsi au kwa biashara.

Muswada huo utakaoendelea kujadiliwa kesho, unaanzisha Bodi ya kuzuia na kudhibiti vileo itakayokuwa na mamlaka ya kutoa vibali kwa mujibu wa sheria, kwa hoteli, baa, maduka, maghala na vibali vya kusambaza vileo katika matukio muhimu.

Sheria hiyo inazuia mtu kuonekana kutoka kwenye baa akiwa ameshika kileo na imeweka masharti mbalimbali ya kumiliki leseni za vileo visiwani humo, yote ikiwa ni katika kupambana na vitendo vya vurugu vinavyosababishwa na walevi wa pombe.

The post Zanzibar: Serikali yapeleka muswada kuzuia biashara ya pombe katika kupambana na vitendo vya vurugu vinavyosababishwa na walevi appeared first on Bongo5.com.