Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetoa wito kwa wananchi kuteketeza Barakoa zao vizuri baada ya kumaliza matumizi yake kisha kuitupa sehemu salama ili kuepusha kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.


.
Wito huo, ameutoa Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona. .
.
“Wale ambao mmevaa Barakoa (mask) zile ambazo zinatakiwa kutupwa baada ya kutumika (disposable mask) , ukumbuke kabla hujaitupa uitoboe ili mtu mwingine asiweze kuiokota na kuisafisha na kuirudisha katika mzunguko jambo litalosaidia kuepusha magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa Corona” alisema. .
.
Alisema, katika baadhi ya nchi imethibitika kuwa, mgonjwa mmoja wa Corona anaweza kuambukiza mpaka watu kumi kwa wakati mmoja hii inatokana na mwingiliano uliopo baina ya watu, hivyo kutoa wito juu ya kuchukua tahadhari kwa hali ya juu.
.
“Kwa baadhi ya nchi zilizopata maambukizi, inasemekana kuwa, mtu mmoja aliyeambukizwa virusi hivi anauwezo wa kuambukiza mpaka watu kumi kwa wakati mmoja” alisema.
.
Aidha, alisema kuwa, kwa wale ambao wanatumia Barakoa za kitambaa, kuhakikisha wanabadirisha mask hizo kila baada ya masaa manne ili kuepusha kupata magonjwa mengine, huku akisisitiza kuwa, ni muhimu kabla ya kuivaa zifuliwe kwa maji na sabuni kisha ipigwe pasi ili kujiweka salama zaidi dhidi ya magonjwa.
.
“Kwa wale ambao mnavaa Barakoa (mask) za kitambaa basi mkumbuke kuwa, mask hiyo inatakiwa ivuliwe kila baada ya masaa manne mpaka sita, na hakikisha kuwa, unaifua kwa maji na sabuni, umeinyoosha ili kama kuna virusi humo waweze kufa, usivae barakoa (mask) ambazo ni chafu” alisema

The post Wizara ya Afya Tanzania “Barakoa yako kabla ya kuitupa, Iharibu kwanza na itoboe” appeared first on Bongo5.com.