Tarehe Saba ya Mwezi April ya kila mwaka ni kumbukumbizi ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Abeid Amani Karume ambapo Familia ya Marehemu Brig. Gen Nnauye imeutambulisha wimbo uitwao “Tunakulilia Karume” wa kumuenzi Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, uliotungwa na Marehemu Brig. Gen Mstaafu Moses Nnauye mwaka 1972 kufuatia kifo cha ghafla cha Rais huyo.

Wimbo huu wa maombelezo ulikuwa ukiimbwa na vijana wa halaika kwa kuongozwa na yeye mwenyewe Brig. Gen Nnauye akipiga kinanda cha mkononi (accordian) kuanzia Bagamoyo alikokuwa Mkuu wa Wilaya na baadaye Singida alikokuwa Mkuu wa Mkoa. Familia ya Marehemu Mzee Nnauye imeona ni vema kutumia siku ya kumbukumbu ya kifo cha Marehemu mpendwa wetu Sheikh Amani Abeid Karume kuutambulisha rasmi wimbo huu kwa kushirikiana na Tanzania House of Talent (THT).

Pamoja na kuwa mwanasiasa mkongwe, Marehemu Brig. Gen Nnauye alipenda sana sanaa na alitumia nyenzo hiyo kuhamasisha harakati za uhuru, kuwahamasisha wanajeshi waliokuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya Nduli Iddi Amini ili wawe na ujasiri wa kushinda vita na hatimaye kuwa na taifa lenye amani na usalama.

Pia alikuwa Mwanzilishi na Mlezi wa vikundi mbali mbali vya Kwaya, Taarabu na Muziki wa Dansi ambapo aliweza kuvumbua vipaji vya wasanii mbalimbali akiwemo Marehemu Capt. Komba, Waziri Ally (Kilimanjaro Band) na wengineo. Katika kuenzi na kuendeleza kile alichokiamini Marehemu Mzee Nnauye katika kutafuta, kusimamia, kulea na kuendeleza vipaji vya sanaa, Familia ya Mzee Nnauye imeona THT ni Taasisi muafaka kushirikiana nayo katika kuhuisha wimbo huu kwani unawiana na malengo ya kituo hicho.

Wimbo huu wenye mahadhi ya Taarabu Asilia (Zanzibar) umerekodiwa upya kwa mara ya kwanza katika studio za THT na Producer Ringtone akishirikiana na Producer Munga wa Time Wrekords, kuongozwa na msanii Lameck Ditto na kuimbwa na wasanii wa THT. Familia ya Mzee Nnauye inapenda kuwashukuru wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha jambo hili kwa ufanisi unaoonekana.

The post Wimbo wa kumuenzi Sheikh Amani Abeid Karume uliotungwa na marehemu Brig. Gen Mstaafu Moses Nnauye na kuimbwa tena na THT (Audio) appeared first on Bongo5.com.