Serikali imewataka wahudumu wa afya nchini kufuata kanuni na miongozo iliyopo katika kutoa huduma kwa wagonjwa kwa kufanya hivyo wataweza kuepuka kupata maambukizi kutoka kwa wagonjwa wanaowahudumia.

Rai hiyo imetolewa leo jijini  jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akipokea msaada wa vifaa vya kunawia mikono 100 vyenye ujazo wa lita 500 kutoka kwa Shirika  lisiyo la kiserikali la Water Mission Tanzania .

Waziri Ummy alisema kama mtaalamu wa afya atafuata mwongozo wa kuzuia maambukizi wa mwaka 2018  na muongozo wa uzuiaji wa maambukizi ya Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) wa mwezi wa kwanza mwaka 2020 hataweza kupata maambukizi kutoka kwa mgonjwa . “Wakati tunaendelea kukabiliana na janga la ugonjwa wa COVID -19  tukumbuke kuwa kuna magonjwa mengine kama ya moyo, kisukari, maralia, figo na ya kuambukiza ikiwemo Ukimwi na kifua kikuu.  Hivyo basi mgonjwa wa aina hii akifika katika kituo cha kutolea huduma za  afya anatakiwa kutibiwa na siyo kukimbiwa”,. “Baadhi ya wahudumu wakimpokea mgonjwa mwenye joto kali wanamkimbia kwa kudhani kuwa  ana ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona. Mwongozo wa utoaji wa huduma za afya hauwataki kuwakimbia wagonjwa jambo la muhimu ni kufuata miongozo iliyopo hii ikiwa ni pamoja na kunawa mikono, kuvaa barakoa na glovu wakati una muhudumia mgonjwa ”, alisisitiza Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy alishukuru kwa msaada uliotolewa na Shirika hilo na kuwataka wananchi kuzingatia maagizo wanayopewa na wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni pamoja na kuvaa barakoa katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Water Mission Tanzania Benjamin Filskov alisema Taasisi yake imetoa msaada huo wa vifaa vya kunawia mikono  100 ambavyo vitatumika katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika mkoa wa Dar es Salaam.

The post Waziri Ummy – Msiwakimbie wagonjwa appeared first on Bongo5.com.