Na Mwandishi Wetu

NI MIAKA 36 sasa tangu atangulie mbele ya haki mwanamapinduzi, mzalendo, shujaa Edward Moringe Sokoine Waziri Mkuu wa pili kwa Tanzania ambaye ameshikilia madaraka hayo kwa nyakati mbili tofauti kuanzia mwaka 1977 hadi 1980 na mwishoni mwa mwaka 1983 hadi mauti yalipomkuta 1984 kwa ajali ya gari pale Mvomero katika kijiji Dakawa Wami au kwa sasa Dakawa Sokoine.

Edward Moringe Sokoine alizaliwa tarehe 01, Agosti 1938 na kufariki tarehe 12, Aprili 1984, anakumbukwa na Watanzania kwa kuwa alikuwa kipenzi cha wanyonge, adui wa wazembe wasiotaka kufanya kazi, wafanya biashara za magendo, wahujumu uchumi waliorejesha na kusalimiisha mali walizojilimbikizia au kuzitupa bila kufuatwa na polisi wala mgambo.

Sauti yake ilikuwa na mamlaka tosha ya kuwaadabisha wale wote walioenda kinyume na maelekezo sahihi ya serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi thabiti wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hakika wema hawana maisha kama ule wimbo wa Patrick Balicidiya wa Afro Sabini Bendi ulioibwa miaka ya 1970 unaosema “Wema hawana maisha” ambapo alikuwa anasikitika kuona viongozi waliotafuta uhuru barani Afrika wamepoteza maisha kwa njama za mabeberu wa Magharibi.

Sauti yake yenye maelekezo aliyoitoa nanukuu “Ole wao wale wanaotumia nafasi zao za umma na serikali, kuiba, kuhujumu uchumi, kupokea rushwa, maana salama yao ni kudra za Mwenyezi Mungu labda nisiwajue"

Waziri Mkuu Sokoine alisema maneno hayo tarehe 12, Aprili 1984 mjini Dodoma wakati wa mkutano wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chake yaani Chama cha Mapinduzi (CCM), wakati huo nchi iliingia kwenye vita kali ya kupambana na walanguzi, wahujumu uchumi, wazembe kazini wenye kufanya biashara za magendo na masuala kama hayo.

Maneno yake yanaonesha jinsi alivyokuwa jabali katika kukabiliana na changamoto za watu ambao wengi walikuwa ni sehemu ya usimamizi wake wa utendaji kazi katika serikali aliyoisimamia . Kutokana na juhudi zako amekuwa kielelezo kwa viongozi wanaochaguliwa nyakati hizi ambao wengine hawamjui ila wanajua historia yake na utendaji wake serikalini uliotukuka.

Yale aliyoyafanya hapa Tanzania ni muongozo sahihi kwa kiongozi bora anayeipenda nchi yake kwa moyo wake wote hakika anastahili kukumbukwa daima na Mwenyezi Mungu alaze roho yako mahala pema peponi.

Ukisikia maadili ya uongozi, Waziri Mkuu Sokoine ndiye aliyekuwa mfano bora kwa uadilifu, unyoofu, utii, uchapakazi, uvumilivu na usikivu kwa wananchi wanyonge ambao wakati huo walikuwa wanapambana na hali ngumu ya kuporomoka kwa uchumi wa dunia pamoja na ule wa Tanzania. Ambapo wafanyabiashara walitumia mwanya huo kuwasulubu raia wanyonge kwa kuficha mahitaji muhimu ya maisha ya mwanadamu na kuapa kuwashughulikia na kweli walitupa shehena za sukari, unga, sabuni, nguo, mafuta ya kula, fedha na vitu kama hivyo barabarani na kuvitelekeza na Watanzania wakiwa wanashangaa kumbe vipo wenzetu wenye fedha wanavificha ili sisi tuhangaike? Hakika wanyonge walimpenda Waziri Mkuu Sokoine kwa moyo wao wote.

Akithibitisha kuwa yeye ni kiongozi anayesimamia haki usawa na kufuata taratibu miongozo na sharia zilizowekwa alisema “Katika nchi inayojali haki na usawa majeshi hayana budi kuwa ni chombo cha kulinda haki na walio wengi na kamwe hairuhusiwi kuwa ni chombo chenye wachache wenye kujali nafsi zao na kusahau masilahi ya walio wengi”

Habari na taarifa ya kifo chake ilikuwa ni pigo na pengo kubwa kwa wapenda maendeleo na wale wote waliokuwa wanapenda kuwatumikia wanyonge wa nchi hii. KIfo chake kilitokana na ajali ya kugongwa na gari lililokuwa likiendeshwa na mkimbizi wa kisiasa kutoka nchini Afrika kusini aliyejulikana kwa jina la Dumisan Dube, iliyotokea eneo la Wami Dakawa sasa kunajulikana kama Wami Sokoine mkoani Mororgoro. 

Mchango wa Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine ni mkubwa katika Taifa hili, alikuwa ni kiongozi anayethamini utu wa mtu na aliamini siasa za Ujamaa na Kujitegemea ndio suluhisho kwa Watanzania kwa kuwa ina manufaa kwa kila Mtanzania kwa kuzingatia usawa. Alijua maendeleo yeyote katika nchi hupatika kwa watu wake kuamua kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka na kukatishwa tamaa na wasioitakia heri nchi yetu.

Aidha, Waziri Mkuu Sokoine alichukizwa sana na vitendo vyovyote vyenye viashiria vya rushwa au rushwa yenyewe, uhujumu uchumi, wafanya magendo ,walanguzi wanaojinufaisha kwa kuwanyonya wananchi wanyonge. Pia, alikuwa ni kiongozi anayetenda yeye mwenyewe bila kumsubiri mtu kumfanyia kazi. Aliamini kilimo ni uti wa mgongo wa taifa hii ambapo mara kwa mara alifanya ziara katika mikoa mbalimbali kuangalia shughuli za kilimo zilivyokuwa zinaendeklea. 

Vilevile alipenda sana na kutunza utamaduni wa kiafrika na ule wa Tanzania hususan kabila atokalo la Wamasai na utaifa wa Mtanzania.Anapotimiza miaka 36 tangu atutoke hapa duniani kwa pamoja Watanzania hatuna budi kujifunza kutoka kwa Mhe. Sokoine na kuhakikisha tunaendeleza nyayo zake za kuwa wazalendo, wapenda haki, kuwa na tabia na desturi ya kufanya kazi kwa bidii na kuipenda kazi, ikiwa ni pamoja na kutumia maarifa tuliyonayo ili tulete tija katika jamiii yetu ya ndani na inayotuzunguka, ikiwa ni pamoja na majirani zetu na wageni wote wanaofika katika nchi hii.

Pia, utamaduni aliotuachia Waziri Mkuu Sokoine ni vema tukaurithisha kwa watoto wetu na vizazi vijavyo kwa manufaa ya Taifa hili na mstakabali wa Taifa letu. Hakuna jambo muhimu na zuri unapoondoka katika dunia hii na kuhakikisha unaacha mfano wa kuonesha umeifanyia nini Tanzania badala ya wewe kuwa sehemu ya kupalilia na kupandikiza viashiria vya chuki, uadui na ubeberu wa kusaliti nchi yako kwa faida ya nchi nyingine.

Edward Moringe Sokoine aliishi maisha ya kawaida kama Mtanzania yeyote yule bila kujali nyadhifa aliyokuwa nao. Wakati wa mazishi yake pale Wilaya ya Monduli Rais Nyerere alisema “Marehemu Sokoine alikuwa na mashati matatu, suruali tatu na jozi mbili tu za viatu, hakuwa na chochote ukiacha ng’ombe alioachiwa na wazazi wake”.

Nisingependa kuongeza chochote lakini wewe unayesoma makala hii unaweza kuwa na majibu kuhusu maisha ya Waziri wetu Mkuu wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hakika atabaki kuwa alama ya uzalendo, uadilifu, unyenyekevu na kujishusha kwa ajili ya kuwatumikia wanachi wanyonge wa Tanzania. Ulale pema peponi daima tutakukumbuka.