SALVATORY NTANDU
Wanaume wawili ambao hawajafahamika Majina wala Makazi wenye umri kati ya 20-25 wanaodhaniwa ni wezi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamepoteza Maisha wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji kahama baada ya kushambuliwa na watu wenye hasira kali baada ya kuwakamata wakiwa na mali zinazodaiwa kuwa ni za wizi.

Kwa Mujibu wa Taarifa iliyotolewa Aprili 20 mwaka huu na Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba imesema kuwa tukio hilo limetokea jana katika Mtaa wa Majengo baada ya kukamtwa na wananchi wakiwa na Televisheni (1)aina ya Tandar na Radio (1) ya Subwoofer mali ya Ayoub Kingi mkazi wa mtaa huo ambazo wanatuhumiwa kuziiba.

“Watu hawa walikamatwa na wananchi wakiwa wamebeba mali hizo zenye thamani ya shilingi laki 345,000 na kisha kushambuliwa kwa kupigwa na mawe sehemu mbalimbali za miili yao na wananchi waliojichukulia sheria na kisha kupelekwa katika hospitali ya Mji kahama  na walifariki dunia wakiwa wanapatiwa matibabu,”alisema Kamanda Magiligimba.

Kamanda Magiligimba alisema kuwa Chanzo cha tukio ni hilo ni wananchi kujichukulia sheria mkononi baada ya kuwatuhumu watuhumiwa kuwa ni wezi na juhudi za kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa waliohusika na tukio hilo zinaendelea.