Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, George Simbachawene ameagiza Mohamed Nangonga ambaye ni mhandisi wa kampuni ya Nangonga Ltd kukamatwa kwa madai ya uzembe wa kutoweka alama za barabarani na kusababisha vifo vya watu watatu. 

Mkandarasi huyo anasimamia kuweka viraka katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma barabara ya Dodoma- Morogoro. 

Akizungumza jana Jumatano Aprili 15, 2020, Simbachawene alisema kampuni hiyo imechimba mashimo katika eneo hilo na kuyaacha muda mrefu bila kuweka alama.

Inadaiwa eneo la Ihumwa ambako ndiko kulikokuwa kukifanyika ukarabati huo juzi kulitokea ajali ambayo iliua watu wawili hapo hapo kutokana na kukwepa shimo.

Pia jana lori lilokuwa limebeba saruji lilokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Kigoma  lilipata ajali ya kugongana na Basi  na hivyo kusababisha kifo cha utingo wa Lori hilo.

Kutokana na ajali hizo,Waziri Simbachawene alifika jana eneo la ajali ambapo alidai Serikali haiwezi kukubali uzembe huo, kwani ajali zimesababishwa na Mkandarasi kutokuweka alama za barabarani wakati akifanya matengenezo.

“Serikali haiwezi kukubali watu wafe tena kwa uzembe hivyo nakuagiza RTO licha ya kwamba huyu ni rafiki yangu mkamate mweke ndani hatuwezi kuwa tunaangalia tu huu uzembe nasema kamata weka ndani pamoja na hawa wafanyakazi wote,”alisema simbachawene.

Mara baada ya kutoa maelekezo hayo Mkuu wa Usalama Barabarani (RTO) Mkoa wa Dodoma,Nuru Selemani alimkamata Mkandarasi huyo na kumpeleka katika gari la Polisi lilokuwepo eneo hilo.

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi,alisema amekuwa akipita katika eneo hilo lakini kumekuwa hakuna alama zozote ambazo zimewekwa kwamba kuna ujenzi unaendelea huku kukiwa na shimo kubwa ambalo limechimbwa.

Alisema Jeshi la Polisi na Wakala wa Barabara (Tanrod) wanatakiwa kutafakari utendaji kazi wao kutokana na uzembe ambao umejitokeza katika neo hilo.

“Nuru (Mkuu wa Usalama Barabarani RTO Mkoa wa Dodoma) hii ni aibu huu ni zaidi ya uzembe mashimo yanachimbwa bila kuwekwa alama yoyote,Tanrod mpo tu mnawaangalia hapa zimetokea zaidi ya ajali nne mnaangalia tu hapana nasema hapana lazima watu wawajibishwe,nimekasirika sana,”alisema.